Quantcast
Channel: MPEKUZI
Viewing all 45270 articles
Browse latest View live

Uswisi yatoa bilioni 18 kuongeza uwajibikaji

$
0
0
Ubalozi wa Uswisi nchini umetoa Sh bilioni 18 kwa asasi za kiraia tatu, zitakozotumika kwa kipindi cha miaka minne ijayo.

Fedha hizo zinalenga kusaidia asasi hizo katika shughuli zao za kuboresha uwazi na uwajibikaji kwenye nyanja mbalimbali nchini. Asasi zilizonufaika na fedha hizo ni Foundation for Civil Society (FCS), Policy Forum na Twaweza.

Akizungumza kwenye shughuli ya kutiliana sahihi ya msaada huo, Balozi wa Uswisi nchini Florence Mattli ameeleza kuwa lengo kuu la msaada huu ni kushiriki katika kukuza uwajibikaji kwenye mamlaka mbalimbali, ili kuboresha sera na huduma za jamii.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza Aidan Eyakuze ameeleza kuwa msaada huo utasaidia taasisi hizo kuendeleza ushirikiano baina yao na serikali.

“Asasi nyingi za kiraia zina mawazo mazuri lakini hazina uwezo wa kuwasilisha mawazo hayo kwenye ngazi husika, msaada huu utatusaidia kuwafikia na kuwawezesha kuwasilisha mawazo ya wananchi,” aliongeza

Mkuu wa Wilaya Igunga Anasa Wanafunzi Wakicheza Kamari Muda wa Masomo

$
0
0
Mkuu wa wilaya ya Igunga, John Mwaipopo ameamuru kutandikwa viboko hadharani wanafunzi sita wa sekondari baada ya kuwakuta wakicheza kamari muda wa masomo.

Wanafunzi walionaswa na mkuu huyo wa wilaya ni wa shule mbili za sekondari zilizopo kata ya Igunga ambao walicharazwa viboko vinne kila mmoja huku wengine wanne wakiwekwa mahabusu.

Akizungumza jana, Mwaipopo alisema akiwa katika ziara ya kugawa na kukagua vitambulisho vya wajasiliamali, mtaa wa Sokoni alikuta vijana 10 wakicheza kamari na alipowahoji sita walibainika ni wanafunzi wa sekondari. Alisema baada ya kuwakamata wanafunzi hao alimuita mkuu wa Shule ya Sekondari Igunga, Renatus Buswelu na kuwatambua watatu ni wa shule yake.

Alisema wanafunzi wengne watatu walibainika ni wa Sekondari ya Mwayunge na alimwita mkuu wa shule hiyo ambaye aliwatambua na kueleza wamekuwa watoro wa mara kwa mara.

Mwaipopo alimwamuru mkuu wa Shule ya Sekondari Igunga, kutoa adhabu ya viboko hadharani ambapo walichapwa vinne kila mmoja huku wananchi wakimpongeza mkuu wa wilaya kwa adhabu hiyo.

Vijana wengine wanne ambao si wanafunzi lakini walikuwa na wanafunzi hao walipelekwa kituo cha polisi Igunga.

Rwanda yawataka raia wake walio karibu na mpaka wa Burundi kusitisha biashara na Burundi

$
0
0
Serikali ya Rwanda imewasihi wananchi wake walioko karibu na mpaka kati ya nchi hiyo na nchi ya Burundi kusitisha biashara yoyote na majirani zao wa nchi ya Burundi.

Hayo yanajiri ikiwa ni siku chache tu baada ya Rwanda kuwakataza wananchi wake kwenda nchini Uganda.Rwanda inashutumu nchi hizo kusaidia makundi ya waasi yanayoipinga.

Wito wa kuwakataza wanchi wa maeneo ya mpaka baina ya Rwanda na Burundi kutokwenda nchini humo umetolewa na afisa katika jeshi la Rwanda Jenerali Mbarac Muganga wakati wa mkutano wa usalama baina yake ,wananchi na viongozi wa maeneo ya mpakani upande wa kusini mashariki.

Jenerali Muganga amewataka kusitisha shghuli zote zinazoweza kuwalazimisha kwenda nchini Burundi hata kama itakuwa ni kuoa au kuolewa na mtu kutoka upande wa pili:

''Majirani wale walituchimbia shimo,kila mnyarwanda anayekwenda huko anatupwa ndani,hii ni kwa mjibu wa taarifa za uhakika tulizo nazo. 

"Hatutawashambulia nchini mwao kwani sisi tunalinda mipaka yetu.Rwanda tunajitosheleza kwa chakula ndiyo maana tunawasihi kutumia kile kidogo tulicho nacho.

"Kuna wengi pia wanaokwenda kuowa au kuolewa upande wa pili wa mpakani si kwamba tunataka kuvunja ndoa zenu lakini tunawasihi kusitisha safari za kwenda huko na vile vile kupunguza wageni mnaopokea kutoka huko kwa sababu wanakuja wakiwa na malengo mengine mengi'' .

Burundi imeishaitangaza Rwanda kama adui wake mkubwa.Nchi mbili zinashutumiana kuunga mkono makundi ya waasi kutoka kila upande.

Miaka 3 iliyopita Burundi ilitangaza kusitisha biashara yake na Rwanda hasa mboga na matunda na pia kusitisha misafara ya mabasi ya abiria kutoka Rwanda.

Rwanda imekuwa na tahadhari kubwa kwenye mipaka yake kutokana na makundi mbali mbali ya waasi yanayotishia kuishambulia.

Hayo yamejiri wakati ambapo Rwanda iliwakataza wananchi wake kwenda nchini Uganda,nchi iliyokuwa na biashara kubwa na Rwanda.

Serikali ilishutumu Uganda kuwanyanyasa wananchi wake wanaokwenda ama kuishi nchini Uganda na pia kusaidia makundi ya waasi wanaotaka kuangusha utawala wa rais Paul Kagame.

Credit:BBC

Jumuiya za watumia maji njombe zatakiwa kutunza mitandao ya maji

$
0
0
Na Amiri kilagalila Njombe
Halmashauri ya wilaya ya Njombe kwa kushirikiana na shirika la maendeleo la nyanda za juu kusini  SHIPO  imeadhimisha kilele cha wiki ya maji  kwa kutoa elimu kwa viongozi wa  jumuiya 22 za watumia maji  za wilaya hiyo ambazo pamoja na kupatiwa elimu ya utunzaji wa miundombinu ya maji na vyanzo pia zimetembelea jumuiya kubwa ya watumia maji ya Tove-Mtwango na kujifunza namana ya kusimamia jumuhia zao.

Wakizumza na mtandao huu  baadhi ya viongozi wa jumuiya za watumia maji kutoka wilayani njombe wamesema kuwa miradi mingi ya maji inakufa na kushindwa kuwa endelevu kutokana na gharama za uchangiaji matumizi ya maji kuwa chini hali inayasababisha miradi kushindwa kujiendesha.

“Kwa ujumla wenzetu wako juu sana tofauti na ninakotoka mimi hata kama mradi wao ni wa mtiririko inaonekana wao maji ni mengi na wenzetu wana kamati ambazo zimekamilika na kila wakati wana vikao namna ya kuendesha huu mradi na kwa ufupi kulingana na vikao wanavyoviweka basi ndivyo maendeleo yao ya uendeshaji wa maji yanavyofanikiwa” alisema TULAWONANA MANGI’TA mwenyekiti wa jumuiya ya watumia maji Ikuna

Kaimu mhandisi wa maji halmashauri ya wilaya ya Njombe Kinganola sanga na Olaisi ole Mgaya mratibu wa miradi ya maji kutoka shirika la shipo wamesema lengo la kufanya ziara katika mradi huo wa tove mtwango ni kutaka viongozi hao wajifunze namna ya  kuendesha  jumuiya katika maeneo yao kwa ubora wa hali ya juu.

“Tumekutana kwa lengo la kuelimishana na kukumbushana Tove mtwango ni jumuiya inayosifika na inafanya vizuri na inatekeleza mradi kwa zaidi ya vijiji 16 vya wilaya ya Njombe na Wanging’ombe  na kwa sababu hiyo ni sehemu nzuri kwa jumuiya zingine kujifunza namna wenzao wanavyo tunza na kulinda mitandao ya maji ili iwe endelevu kwa vizazi vya sasa na vijavyo”walisema KINGANOLA SANGA na OLAISI OLE MNGAYA mratibu wa miradi ya maji Shipo.

Jumuiya ya watumia maji ya Tove- Mtwango ina vijiji 16 na iliasisiwa tangu mwaka 2008 baada ya mradi huo wa maji  kukamilika uliojengwa  kwa ufadhili wa kanisa katoriki kwa kushirikiana na  serikali ambapo jumuiya hiyo imetajwa kuwa na  mipango mizuri ya usimamizi.

“Kwa kweli tumejipanga sasa kuhakikisha tunafunga mita kwa ajili ya vituo vyetu vya maji kwa sababu havina maji na tutafanya hivi ili kuhakikisha hakuna tone lolote la maji litakalopotea”alisema ABDALA MTEMI meneja wa jumuiya ya watumia maji Tove mtango.

Naibu waziri ulega asisitiza ukuaji wa sekta ya maziwa mkoani tanga

$
0
0
Na. Edward Kondela
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega amefanya ziara ya siku moja Mkoani Tanga na kukutana na mkuu wa mkoa huo Bw. Martine Shigella pamoja na kuzungumza na wanachama wa Chama Kikuu cha Ushirika wa Maziwa Mkoa wa Tanga (TDCU).

Mara baada ya kufika katika ofisi ya mkuu wa mkoa wa Tanga, Mhe. Ulega alipokea taarifa ya mkoa iliyoainisha pia changamoto zilizopo katika sekta ya mifugo na uvuvi mkoani humo, ambapo Bw. Shigella ameiomba Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuzidi kutoa elimu kuhusu operesheni mbalimbali ambazo zinafanywa na wizara hiyo ili kuondoa usumbufu ambao umekuwa ukijitokeza kwa wananchi hususan kwa wanaofanya shughuli za uvuvi katika mwambao wa Bahari ya Hindi.

“Niiombe Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia kwako mhe. naibu waziri kumekuwa na operesheni ambazo zinafanyika mara kwa mara na wakati mwingine watu kulalamika kuonewa, ni vyema operesheni hizi zikaenda sambamba na utoaji wa elimu ili kuondoa malalamiko ya wananchi.” Alisema Bw. Shigella

Aidha Bw. Shigella amemfahamisha Naibu Waziri Ulega ushirikiano kati ya Tanzania na Rwanda ni fursa kubwa ya kuwezesha uzalishaji wa maziwa katika Mkoa wa Tanga kupitia matumizi ya bandari na ubia na kiwanda cha Tanga Fresh, hivyo wizara haina budi kuwawezesha wafugaji kupata ng’ombe wa kisasa ili kuzalisha maziwa kwa wingi na kufaidika na ushirikiano huo.

Akibainisha hatua mbalimbali za Wizara ya Mifugo na Uvuvi katika kuboresha sekta ya maziwa kwa mkuu wa mkoa wa Tanga, Naibu Waziri Mhe. Abdallah Ulega amesema fursa mbalimbali zinazojitokeza mkoani Tanga ikiwemo ujumbe kutoka Rwanda kutumia bandari ya Tanga na kuweka ubia na kiwanda cha Tanga Fresh kutasaidia kukuza sekta ya maziwa mkoani humo.

“Kupitia uwekezaji huu uzalishaji wa maziwa utaongezeka na hivyo kuimarisha uchumi na kipato cha mwananchi kwa kuwa mahitaji ya maziwa yataongezeka hivyo lazima kuhamasisha zaidi ufugaji wa kisasa na wenye tija.” Alisema Mhe. Ulega

Aidha Mhe. Ulega amesema kuhusu operesheni mbalimbali zinazofanywa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kulalamikiwa na baadhi ya watu kuonewa, amesema masuala ya operesheni yanafanyika kwa mujibu wa sheria na kwamba kuna baadhi ya mambo ambayo yanajitokeza katika operesheni hizo hivyo yanafanyiwa utafiti ili kuainisha yale ambayo yataonekana hayaendani na hali halisi ya wakati huu.

Katika hatua nyingine, mara baada ya kikao na Mkuu wa Mkoa wa Tanga Bw. Martine Shigella, Naibu Waziri Ulega alipata fursa ya kutembelea kiwanda cha maziwa cha Tanga Fresh na baadae kuzungumza na wanachama wa Chama Kikuu cha Ushirika wa Maziwa Mkoa wa Tanga (TDCU).

Akizungumza na wanachama hao Mhe. Ulega amebainisha kuwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia Dawati la Sekta Binafsi imeiuanganisha Benki ya Kilimo (TADB) na TDCU kutoa mikopo ya ng’ombe takriban 300 kwa wafugaji wa Mkoa wa Tanga ili kukuza uzalishaji wa maziwa katika mkoa huo.

“Tuna nia ya kuwawezesha zaidi wafugaji na sisi kupitia Dawati la Sekta Binafsi lililoanzishwa mwezi Oktoba mwaka jana, tuliwapatia lengo la kuhahakisha tunazalisha kiwango cha upatikanaji wa maziwa katika taifa letu na kufanikisha mkopo kati ya TADB na TDCU ambapo sasa mnakwenda kupata ng’ombe bora kabisa takriban 300.”

Aidha Mhe. Ulega amewataka wafugaji kuhakikisha wanatunza mifugo yao vyema na kuwapatia chanjo ili waweze kupata maziwa bora ambayo ndiyo yatawezesha kiwanda cha Tanga Fresh kuzidi kukua na kutoa bidhaa bora zaidi zitokanazo na maziwa.

Naye Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika wa Maziwa Mkoa wa Tanga (TDCU) Bw. Hamisi Mzee amemwambia Naibu Waziri Ulega kuwa chama kinahakikisha kiwanda cha Tanga Fresh kinazidi kuimarika kwa kufuata kanuni za ubora wa maziwa tangu yanapotoka kwa ng’ombe hadi kufika kiwandani hapo.

Amesema uwepo wa kiwanda hicho ni fursa pekee kwa wakazi wa Mkoa wa Tanga na maziwa hayo yamekuwa sehemu ya vitambulisho vikuu vya mkoa huo katika maeneo mbalimbali ndani na nje ya nchi.

Mwisho.

CUF Kuwapeleka Mahakamani Waliochoma Bendera na Kadi za CUF

$
0
0
Chama cha Wananchi (CUF), Wilaya ya Tanga, kimefungua kesi mahakamani kwa ajili ya kuwachukulia hatua za kisheria waliokuwa wanachama wa chama hicho waliohamia Chama cha ACT- Wazalendo kwa madai ya kuchoma bendera na kadi za chama hicho.

Hayo yalibainishwa jana kwenye kikao maalumu kilichoshirikisha wanachama na madiwani wa chama hicho ambao walikuwa na ajenda ya kujadili mustakabali wao baada ya aliyekuwa Katibu Mkuu wake, Maalim Seif Sharif Hamad, kuhamia ACT Wazalendo mapema wiki hii.

Akizungumza baada ya kikao hicho, Naibu Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa CUF Taifa, Masoud Mhina, alisema dhumuni la kikao hicho ni kujitathmini na kuchukua hatua kwa wale waliochoma bendera na kadi kitendo ambacho ni kinyume cha sheria.

Mhina alisema kikao hicho cha kamati tendaji pia kimetoa tamko la kumtaka aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho, Mkoa wa Tanga, Rashidi Jumbe, kuhakikisha mali zote za CUF  alizokuwa anazishikilia anazirudisha kabla hatua kali hazijachukuliwa dhidi yake.

Alisema miongoni mwa mali za chama hicho zinazoshikiliwa na Jumbe ni pamoja na pikipiki tatu, spika, samani za ofisi na mafaili.

 “Tunaheshimu maamuzi yao ya kujiunga na chama mbadala, lakini kuhama kwao hakuhalalishi kuondoka na mali za chama chetu, mali zote za CUF zirejeshwe kwa mustakabali wa chama hicho,” alisema.

Kuwa Wakwanza Kupokea Habari Zetu....Download App Yetu Kwa Kubonyeza Hapa, Huhitaji tena kuwa na Computer

$
0
0
Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa urahisi kabisa kupitia simu yako ya mkononi muda wowote hata usiku wa manane au ukiwa kazini...

Pata kurasa za mbele Magazetini, habari za kitaifa, matukio yote ya kisiasa, burudani na udaku   kupitia simu yako ya mkononi.

Huhitaji tena kuwa na Computer. Ingia Play Store, pakua App yetu  tukuhabarishe masaa 24.

Waziri Mkuu Afanya Mazungumzo Na Balozi Wa Zambia, Italia

$
0
0
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Tanzania nchini Zambia, Mheshimiwa Balozi Hassan Simba Yahya, ambapo amemtaka akaimarishe mahusiano baina ya nchi zote mbili.

Amekutana na Balozi Yahya leo (Jumamosi, Machi 23, 2019) katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Magogoni jijini Dar es Salaam. Waziri Mkuu pamoja na mambo mengine amemtaka balozi huyo kuhakikisha anaboresha shughuli za Kidiplomasia kati ya Tanzania na Zambia.

Pia, Waziri Mkuu amemtaka akakutane na wafanyabiasha wa Zambia na awahamasishe waje wawekeze katika sekta mbalimbali ikiwemo ya viwanda. Amesema Balozi huyo anaweza kuandaa kongamano la biashara na uwekezaji kwa kuwakutanisha wafanyabiashara na wawekezaji wa Tanzania na Zambia ili kuboresha uchumi.

Kwa upande wake, Balozi Yahya amesema atahakikisha anayafanyia kazi maelekezo yote aliyopewa ikiwa ni pamoja na kuimarisha biashara pamoja na kuboresha ushirikiano baina ya Tanzania na Zambia.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewakaribisha wawekezaji kutoka nchini Italia waje wawekeze nchini na Serikali itawapa ushirikiano wa kutosha. Ameyasema hayo leo alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Italia nchini, Balozi Roberto Mengoni.

Akizungumza na Balozi huyo Ofisini kwa Waziri Mkuu, Magogoni, Dar es salam, Waziri Mkuu amesema Tanzania ipo tayari kuwapokea wawekezaji kutoka kwenye nchi hiyo. “Serikali imedhamiria kuendeleza sekta ya viwanda nchini ili kukuza uchumi na kufikia wa kati ifikapo 2025, hivyo tunawakaribisha wafanyabiashara waje wawekeze”.

Amesema Tanzania iko tayari wakati wote kutoa ushirikiano ili kuhakikisha wawekezaji watakaojitokeza kuwekeza nchini wanafanikiwa ili mataifa yote yaweze kufaidika, ambapo Ofisi yake kupitia Waziri mwenye dhamana ya Uwekezaji, Bibi Angela Kairuki yuko tayari kuwasikiliza na kuwasaidia wawekezaji wote wanaokusudia kuwekeza nchini.

Naye, Balozi Mengoniameishukuru Serikali kwa ushirikiano mzuri uliopo baina ya Tanzania na Italia, hivyo amemuhakikishia Waziri Mkuu kwamba watauendeleza na amesema wapo tayari kushirikiana na Tanzania kuhakikisha mkakati wa Serikali wa kukuza uchumi kupitia sekta ya viwanda unafanikiwa.

(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,

Mradi wa majitaka Mwanza wavutia wageni kutoka nchi mbalimbali ulimwenguni.

$
0
0
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Jijini Mwanza (MWAUWASA) imepokea ugeni kutoka Asasi zisizo za Kiserikali kutoka Brazil, Afrika Kusini, Kenya na Uganda ambao umevutiwa na ubunifu uliyotumika katika ujenzi wa mradi wa Mfumo rahisi wa uondoshaji majitaka kwenye maeneo ya milimani unaofahamika kitaalam kama 'Simplified Sewerage System'.

Hayo yamebainishwa Machi 22, 2019 na Mkurugenzi wa Shirika lisilo la Kiserikali linalojishughulisha na masuala ya Kijamii nchini (CCI) Dkt. Tim Ndezi ambaye alikuwa mwenyeji wa ugeni huo kwa hapa nchini.

Dkt. Ndezi alisema mradi wa majitaka wa simplified sewerage umeendelea kuwa kivutio kikubwa kwa mataifa mbalimbali kote ulimwenguni.

Alisema taasisi zinazojishugulisha na masuala ya usafi wa mazingira kutoka nchi mbalimbali baada ya kupata sifa za mradi huo wa Mwanza zimevutika kujifunza zaidi ubunifu uliotumika katika utekelezaji wake ili pia kuutumia katika nchi wanazotoka.

"Wageni hawa wamekuja kujifunza namna ambavyo mradi huu umejengwa ili nao wakaandae mradi wa namna hii kwenye nchi zao," alisema Dkt. Ndezi.

Mradi huo wa Simplified Sewerage umeendelea kutembelewa na wageni kutoka mataifa mbalimbali kwa lengo la kujifunza namna ukivyotekelezwa na namna ambavyo unaendeshwa.

Kwa mujibu wa Dkt. Ndezi ni kwamna ugeni huo vilevile ulilenga kuzungumza na wanufaika wa mradi huo ili kufahamu wajibu wao na namna ambavyo waliupokea na njia wanazotumia kuutunza.

Hii ni mara ya pili kwa mwaka huu 2019 mradi huo kutembelewa na ugeni kutoka nje ya nchi kwani hivi karibuni MWAUWASA ilipokea ugeni kutoka Kenya ambao ulifika kwa ajili ya kujifunza namna bora ya kutekeleza mradi wa majitaka hususan kwa maeneo yasiyo rasmi.

Ugeni huo wa awali kutoka Nchini Kenya ulieleza namna ulivyovutiwa na ubunifu mkubwa uliyotumika katika ujenzi wa mradi wa majitaka kwenye maeneo ya milimani na kuahidi kurejea tena na wataalam wa mamlaka zinazohusika ili kujenga miradi ya namna hiyo nchini mwao.

Akizungumza mmoja ya wageni hao kutoka Uganda, Mundamba Omar alisema nchini humo ipo changamoto ya wananchi hususan wa kipato duni kukosa mfumo bora na rasmi wa uondoaji wa majitaka na kwamba ziara hiyo waliyoifanya Jijini Mwanza imewapatia uzoefu na ujuzi wa namna ya kujenga na kusimamia mradi mzuri wa majitaka.

"Tunaipongeza MWAUWASA, kazi iliyofanyika hapa ni ya kipekee hatuna budi nasi kuiga," alisema Omar. 

Itakumbukwa kuwa Mradi huo wa Simplified Sewerage ulikuwa miongoni mwa miradi miwili bora zaidi kuwahi kutekelezwa Barani Afrika chini ya ufadhili wa African Infrastructure Trust Fund (EU-AITF).

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendeji wa MWAUWASA, Mhandisi Anthony Sanga ujenzi wa mradi huo ulianza Mwaka 2016 na umenufaisha Kaya zipatazo 415.

Mhandisi Sanga alisema mradi huo wa Simplified Sewerage ulijengwa kwa majaribio kwenye maeneo matatu ambayo ni Kilimahewa, Mabatini na Igogo.

Katika maeneo hayo matatu, Mhandisi Sanga alisema mwitikio ulikua mzuri na alitolea mfano kwa Kilimahewa ambapo MWAUWASA ilipanga kuunganisha Kaya 68 lakini kutokana na mwitikio kuwa mkubwa Kaya 117 ziliunganishwa na kwa upande wa Mabatini mpango ulikua ni kuungnisha Kaya 88 hata hivyo zaidi ya Kaya 178 ziliunganishwa na kufikia jumla ya Kaya 415 kwenye maeneo yote matatu.

Hata hivyo Mhandisi Sanga anabainisha kwamba awamu ya pili ya ujenzi wa mradi huo itahusisha maeneo mengi zidi ambayo ni Kabuhoro, Ibungilo, Kawekamo na Isamilo.

"Maeneo ambayo tulianza nayo kwenye awamu ya kwanza nayo hatujamaliza, kwahiyo haya ni maeneo mapya lakini pia tutarudi kwenye hayo maeneo ya awali tukaunganishe Kaya zilizosalia," alibainisha Mhandisi Sanga.

Akielezea sababu za mradi huo kuitwa simplified, Mhandisi Sanga alisema kwamba mradi ulipunguza baadhi ya vigezo kwenye miongozo ya usanifu miradi kutoka Wizara ya Maji.

"Ukivifuata vigezo vyote kama vilivyo kwenye miongozo inakua ngumu kutekeleza mradi kwenye maeneo ya namna hiyo," alisema Mhandisi Sanga. 

Aliongeza kwamba changamoto iliyopo kwenye Jiji la Mwanza ni kwamba zaidi ya asilimia 70 ya maeneo hususan ya milimani hayajapimwa na hivyo kusababisha ujenzi wa miradi kuwa mgumu.

Alibainisha kwamba kwa Tanzania, Jiji la Mwanza ni la kwanza kutekeleza miradi ya namna hiyo na kwamba kwa duniani miradi ya namna hiyo inapatikana Nchini Brazili.

Mhandisi Sanga alisema lengo mahsusi la mradi huo ni kuondosha majitaka kwa njia rahisi kutoka kwenye maeneo ya milimani ili kuwaepusha wakazi na maradhi yanayoweza kutokea kutokana na mfumo usio rasmi wa uondoshaji wake.

"Lazima tuhakikishe majitaka yanatolewa na yanatibiwa kwakuwa haya yanaweza kuwa ni hatari kwani mara nyingine hua ni chanzo kikuu cha maradhi," alisema.

Alimalizia kwamba hapo awali uondoshaji wa majitaka kwenye maeneo ya milimani Jijini Mwanza ulionekana kuwa mgumu na kutowezekana." Ni lazima tuwe na majawabu kwenye maeneo ambayo hapo zamani ilionekana hayawezekani kabisa," alisema Mhandisi Sanga.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Mbugani, Athumani Jama alisema hapo zamani kabla ya mradi hali ilikuwa ni chafu hasa ikizingatiwa hali halisi ya kijiografia ya maeneo hayo ya milimani.

“Walikuwa wakichimba vyoo vifupi na wakati wa mvua hali inakuwa tete sana, maji yalikuwa yanatiririka ovyo na magonjwa ya mlipuko yalikuwa ya kufikia tu,” alisema Jama.

Wananchi waliozungumza wakati wa ziara ya ugeni huo waliiomba MWAUWASA kuharakisha ujenzi wa mradi mpya ili Kaya nyingi zaidi zinufaike.

Waziri Mkuu Awahamasisha Watanzania Wajitokeze kwa Wingi Kuishangilia Taifa Stars Kesho

$
0
0
Pichani ni Mheshimiwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa  akiwahamashisha Watanzania kujitokeza kwa wingi kesho Jumapili March 24, kuishangilia Taifa Stars katika mchezo wake dhidi ya Timu ya taifa ya Uganda.

Matokeo ya ushindi dhidi ya Uganda yanaweza kuipa Stars nafasi ya kufuzu kwa fainali za AFCON 2019 zitakazofanyika mwezi Juni nchini Misri.

Hata hivyo ili Stars iweze kufuzu lazima Cape Verde iifunge au itoke sare na Lesotho. Mchezo baina ya timu hizo utapigwa huko Cape Verde muda sawa na mchezo kati ya Stars dhidi ya Uganda utakaopigwa kesho saa 12 jioni

Wapinzani wa Stars, Uganda Cranes wanatarajiwa kuwasili nchini leo. Uganda iliweka kambi ya wiki moja nchini Misri kujiandaa na mchezo huo

Waziri Mkuu Atembelea Kambi Ya Stars .......Kamati Yaahidi Milioni 10 Kwa Kila Mchezaji, Iwapo Watavuka

$
0
0
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametembelea kambi ya wachezaji wa timu ya Taifa na kuwaeleza kwamba Serikali na wananchi wanamatumaini makubwa kwa timu yao, hivyo wahakikishe wanapata ushindi katika mechi yao dhidi ya timu ya Taifa ya Uganda.

Pia, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuipongeza Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo pamoja na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa maendeleo makubwa yanayoendelea kupatikana katika soka nchini.

Waziri Mkuu ametembelea kambi hiyo leo (Jumamosi, Machi 23, 2019) jijini Dar es Salaam na amewaeleza kuwa Serikali inaimani nao na kwamba wasiwe na wasiwasi kwa sababu hawana tofauti yoyote na wachezaji wa timu nyingine duniani.

“Macho yote ya Watanzania yameelekezwa katika mechi ya kesho na Serikali inamatumaini makubwa na timu ya Taifa, hivyo waelewe kwamba kesho ni siku muhimu sana. Lengo letu ni kufikia hatua ambayo mataifa mengine yamefikia”.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Saidia Taifa Stars Ishinde na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amesema kamati yake itatoa sh. milioni 10 kwa kila mchezaji wa timu hiyo iwapo timu itafuzu kucheza michuano ya Mataifa ya Afrika (AFCON)

Makonda amesema Watanzania wanachokijua kwa sasa ni kwamba AFCON 2019 ni zamu yao, hivyo amewaomba wachezaji wa timu ya Taifa wahakikishe wanawapa furaha kwa kuifunga timu ya Taifa ya Uganda na kwamba wananchi wengi wamehamasika kwenda kuwashangilia.

Nae, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangala ameahidi kuwapeleka katika mbuga ya wanyama kwa ajili ya mapumziko iwapo wachezaji hao wataibuka na ushindi katika mechi yao dhidi ya timu ya Taifa ya Uganda hapo kesho.

Dkt. Kigwangala amesema Serikali ipo pamoja na wanamichezo, ambapo amewataka wachezaji hao wa timu ya Taifa wakapigane kweli kweli kwa ajili ya Taifa lao. “Kesho muingie uwanjani kama askari wa nchi. Mkapiganie ushindi wa Taifa letu”.

Awali, Nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samata amesema,”Ninafuraha si kwa sababu ya ukubwa wa mechi ya kesho bali ni kwa sababu naona kesho nakwenda kuongoza nchi. Tupo tayari kuliletea Taifa ushindi”.

(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,

Meya wa Manispaa ya Ilala Charles Kuyeko(CHADEMA) amejiuzulu leo Machi 23 Na Kuhamia CCM

$
0
0
Meya wa Manispaa ya Ilala jijini Dar es Salaam, Charles Kuyeko (Chadema)  leo Jumamosi Machi 23, 2019 ametangaza kujiuzulu uanachama wa Chadema na kujiunga na CCM.

Kuyeko ambaye ni diwani wa Bonyokwa amesema anamshukuru Rais wa Tanzania, John Magufuli Kwa kazi ya ajabu ya kutukuka ambayo anaifanya na kuomba Watanzania kumuunga mkono. 

 "Rais Magufuli ni mtu wa kuigwa, anastahili sifa na kazi ya kutukuka, nawaheshimu Viongozi wa CHADEMA kwa kunipa nafasi, nawashukuru na nitaendelea kuwaheshimu lakini mapenzi yangu ya dhati ni CCM" Amesema

Habari Zilizopo Katika Magazeti ya Leo Jumapili ya March 24

Waziri Biteko Asema Wizara Iko Tayari kuwahudumia Watanzania kutokea Ihumwa

$
0
0
Viongozi Waandamizi wa Wizara ya Madini, wakiongozwa na Waziri wa Madini, Doto Biteko jana Machi 23, wametembelea Jengo la Wizara ya Madini lililopo mji wa Serikali eneo la Ihumwa, Jijini Dodoma kwa lengo la kukagua maendeleo ya ujenzi huo.

Akizungumza baada ya kukagua jengo hilo, Waziri wa Madini Doto Biteko amewahakikishia watanzania wote pamoja na wadau wa madini kuwa, wizara iko tayari kuwahudumia kutokea eneo hilo la Ihumwa pindi itakapohamia na kuwataka watumishi kujiandaa kuhamia eneo hilo mara baada ya mkandarasi kukabidhi jengo kwa wizara. 

Vilevile, Waziri Biteko amezitaka taasisi nyingine zenye uhitaji wa kutumia madini ya mawe yanayopatikana nchini ikiwa ni pamoja na mable, kuwa wizara iko tayari kuwasaidia kwa kuwaunganisha na wajeta wake.

Pia, amemshukuru Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa kutokana na msukumo alioutoa kuhakikisha ujenzi wa majengo ya serikali unakamilika kwa wakati. Aidha,  amempongeza Mkandarasi kampuni ya Mzinga Holding Co. Ltd kutokana na kuongeza kasi ya ujenzi ikiwemo kuzingatia ubora nakuongeza kwamba, wizara imeridhika na ujenzi.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo, ameeleza kuwa, wizara imepanga kulifanya eneo la ofisi hiyo kuwa kijani kwa kuhakikisha inapanda miti ya aina mbalimbali na kuhakikisha kwamba eneo hilo linawekewa mazingira mazuri ya kuvutia.
Naye, Katibu Mkuu wa Madini, Prof. Simon Msanjila Amesema Mkandarasi Kampuni ya Mzinga Holding Co. Ltd imeahidi kuikabidhi Wizara jengo hilo ndani ya kipindi cha siku Tano zijazo “awali ujenzi ulianza kwa kusuasua lakini sasa uko katika hatua nzuri na mkandarasi amezingatia ubora,” amesema Prof. Msanjila.
 
Akizungumzia mahitaji ya ofisi na idadi ya watumishi, amemsema kwa idadi ya watumishi wa wizara Makao Makuu ofisi zilizopo katika jego hilo zinatosheleza mahitaji na kuongeza kuwa, kwa kuanza Idara zote na Vitengo vya Wizara vinatarajia kuhamia katika eneo hilo isipokuwa Idara ya fedha kutokana na masuala ya mfumo wa kifedha. Pia, ameeleza kuwa, wizara imetumia malighafi inayopatikana nchini yakiwemo madini ya mable ambayo yamepatikana kutoka kwa wachimbaji wadogo wa madini nchini.

Kwa upande wake, Mkandarasi wa kampuni hiyo   Hamisi Msangi ameihakikishia wizara kuwa , ndani ya siku tano zijazo, jengo hilo litakabidhiwa rasmi kwa wizara hiyo.

Waganga wa kienyeji Kufyagiwa Sumbawanga Baada ya Mauaji ya Watoto Wawili

$
0
0
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa mh. Joachim Wangabo amemuagiza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa ACP Mathias Nyangi kuhakikisha anafanya msako wa waganga wa kienyeji katika mkoa na kuwakamata wale wote wanaofanya uganga wa kienyeji bila ya kuwa na leseni halali za kuwaruhusu kufanya shughuli hizo.

Ametoa agizo hilo baada ya kusikiliza vilio vya wananchi wakati wa mkutano ulifanyika mtaa wa Vuta, Kata ya Kizwite, mjini Sumbawanga, wananchi waliokuwa wakiomboleza vifo vya watoto wawili na mmoja kubaki mahututi katika hospitali ya rufaa ya mkoa baada ya mganga wa kienyeji kuwateka na kuwaficha katika gari lake chakavu tangu watoto hao kupotea tarehe 21.3.2019 na wawili kupatikana wakiwa wamefariki tarehe 23.3.2019 baada ya mmoja aliyepona kutoroka na kuwajulisha wananchi kilichotokea.

Amesema kuwa msako huo wa waganga wa kienyeji ufanyike katika wilaya zote tatu za mkoa ili kuwahakikishia wananchi amani na utulivu ambayo imekuwepo kwa miaka yote na kuwataka wananchi kutoa ushirikiano katika kuhakikisha wanawafagia waganga hao wanaonyesha dalili za kuvuruga utulivu uliopo katika mkoa.

“RPC fanya Operesheni kali ya waganga wa Kienyeji ndani ya Mkoa huu, wale ambao wana leseni tutajua hukohuko kwamba huyu ana leseni n ani halai au siyo halali na kama sio halali basi huyo ni halali yako, na kama kuna mganga wa kienyeji asiye na leseni, huyo ndio kabisa halali yako zaidi, kuanzia sasa hivi bonde la ziwa Rukwa kule Nkasi, Kalambo, Sumbawanga yenyewe hapa kote, opresheni ipite ya kamatakamata waganga wa kienyeji, tumechoka,” Alisisitiza.

Wakati wakitoa malalamiko yao kwa mkuu huyo wa mkoa, wananchi hao walisema kuwa vifo vya watoto hao vinahusishwa na Imani za kishirikina ambapo kumekuwa na wimbi la vijana wanaoonekana wakila, wakinywa na kuvaa vizuri bila ya kujulikana shughuli zao maalum wanazofanya jambo mbalo limekuwa likiwaumiza kichwa wananchi hao na kukosa majibu.

Mmoja wa wananchi hao Debora Maenge alisema “ Nasikitika kwa tukio hili lililotokea mtaa wa Vuta, huyu mtu tunaishi nae jirani sana, tunajua ni mtu mwema, kumbe ni mtu ambae sio mwema na hafai kabisa katika jamii, cha kushanga alikuwa na vibali ambavyo alikuwa akijitambulisha kuwa yeye ni mganga wa jadi, vibali hivi vinatolewa serikalini, Je serikali yetu mtaendelea kutoa vibali hivi ili watu waendelee kuuawa kiasi hiki? serikali angalieni mnapotoa vibali je ni waganga Kweli?” Aliuliza.

Mh. Wangabo alitembelea eneo la nyumba ya mganga huyo wa kienyeji ambayo gari alilowafichia watoto ilikuwamo na kukuta nyumba hiyo ikiwa imevunjwa na gari la mganga huyo kuchomwa moto na wananchi wenye hasira kali.

Watuhumiwa James Kapyela (52) pamoja na mtoto wake Michael Martin (14) wa tukio hilo la mauaji ya watoto Nicolous Mwambage (7) pamoja na Emanuel Juma (4) hivi sasa wanashikiliwa na polisi huku uchunguzi wa awali ukionyesha watoto hao walifariki kwa kukosa hewa baada ya kufungiwa ndani ya gari chakavu aina ya Chaser Saloon iliyokuwa haitumiki na vioo vya gari hiyo kufungwa.

Naibu Waziri Kanyasu Aahidi Kuboresha Makumbusho Ya Mwl.nyerere Butiama

$
0
0
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii,Mhe.Constantine Kanyasu amesema Wizara kupitia Taasisi zake imejipanga kukikarabati na kukiendesha Kituo cha Makumbusho ya Mwalimu Nyerere, kwenye makazi ya Baba wa Taifa wilayani Butiama mkoani Mara.

 Amesema hatua hiyo inalenga kukiboresha kituo hicho ili kiweze  kuwavutia watalii wengi zaidi kutoka ndani na nje ya nchi.

Akizungumza mara baada ya kutembelea kituo hicho wilayani Butiama mkoani Mara,  Mhe. Kanyasu amesema Makumbusho hiyo  ni hazina ya Taifa kutokana na uwepo wa mikusanyo na historia iliyobeba taswira ya Taifa la Tanzania  kabla na baada ya Uhuru.

Amesema yeye akiwa Naibu Waziri  atahakikisha Makumbusho hiyo inatengewa bajeti ya kutosha ili kuiwezesha kuwa ya kisasa na yenye kuwavutia watalii.

Ameeleza  kuwa nchi mbalimbali duniani ikiwemo China zimekuwa zikiingiza fedha nyingi kupitia Makumbusho za viongozi ambao walikuwa  waasisi wa nchi hizo kama alivyokuwa Mwl.Nyerere.

Amesema sifa aliyokuwa nayo Mwl. Julius Kambarage Nyerere lazima iakisi Makumbusho yake kwa kuwa bora na yenye kuwavutia watalii.

Makumbusho hiyo lazima iwekewe mazingira mazuri ili  iakisi utu na uzalendo wake kwa taifa la Tanzania.
 Aidha, amesema Makumbusho hiyo itafanyiwa utaratibu wa kuwa na watumishi wa kutosha wa kuihudumia.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Makumbusho hiyo, Emamuel Kiondo  amemweleza Naibu Waziri huyo kuwa  kituo hicho kina watumishi wawili pekee walioajiriwa na  wengine wakiwa  watumishi wa kujitolea.

Aidha, ameeleza kuwa kituo hicho kinakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ya uhaba wa vitendea kazi.

Waziri Lugola Ataka Biashara Haramu Ya Binadamu Idhibitiwe

$
0
0
Na Felix Mwagara, MOHA-Zanzibar.
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, ameitaka Sekretarieti ya Kitaifa ya Kuzuia na Kupambana na Biashara Haramu ya Usafirishaji wa Binadamu nchini, iongeze kasi ya kupambana na biashara hiyo ili iweze kudhibitiwa kwa kuwa inaichafua nchi.

Waziri Lugola, ambaye kesho anatarajia kufungua mkutano mkubwa wa mafunzo kwa watekelezaji wa sheria ya kuzuia biashara hiyo haramu, katika hoteli ya Ngalawa, mjini Unguja, Zanzibar, alisema wakati akijiandaa kufungua mafunzo hayo, lakini wahusika waweke mikakati thabiti ya kuidhibiti biashara hiyo.

Mafunzo hayo ambayo ni ya siku tano, yatatolewa kwa wadau wanaotekeleza sheria ya kuzuia na kupambana na Biashara hiyo, Maafisa Polisi, Uhamiaji, waendesha mashtaka, Mahakimu, Maafisa Ustawi Jamii na Mashirika yasiyokuwa ya Kiserikali (NGO’s) yaliyopo Zanzibar.

Akizungumza na Mwandishi wa habari hii, Waziri Lugola alisema Mkutano huo ni muhimu kwa wadau hao kupata mafunzo ya kukabiliana na mapambano ya biashara hiyo haramu ambayo Wizara yake itaendelea kuidhibiti. 

“Nimealikwa kufungua mkutano huo, baada ya mafunzo hayo ya kitaalamu ambayo nimeambiwa yatakuwa ya siku tano, naamini maafisa watakaopewa mafunzo hayo kutoka Wizara yangu na maafisa wengine wa Serikali kutoka sehemu mbalimbali nchini, pamoja na NGO’s za hapa Zanzibar watakuwa wamepikwa na kuiva na hatimaye watatusaidia katika kutekeleza sheria ya kuzuia biashara hii haramu ya usafirishaji wa binadamu,” alisema Lugola.

Kwa upande wake, Katibu wa Sekretarieti ya Kitaifa ya Kuzuia na Kupambana na Biashara hiyo Haramu kutoka Wizara hiyo, Separatus Fella, alisema zaidi ya washiriki 80 watapewa mafunzo hayo na anamatarajio makubwa elimu watakayopewa itazaa matunda.

Fella alisema washiriki watapewa mafunzo mbalimbali katika semina hiyo itakayofanyika Kesho Machi 25, 2019, ambapo mada mbalimbali zitawasilishwa zikiwemo, washiriki kujua kutofautisha makosa ya biashara haramu ya usafirishaji binadamu na mengine, na namna ya kupeleleza na kuendesha mashtaka.

“Pia washiriki watajifunza namna ya kuwalinda na kuwasaidia wahanga wa biashara haramu ya usafirishaji binadamu, namna ya kuhoji watuhumiwa na mashahidi kwenye kesi za biashara haramu ya usafirishaji Binadamu,” alisema Fella.

Aidha, katika ufunguzi wa mafunzo hayo ambayo mgeni rasmi atakuwa Waziri Lugola, Fella alisema pia maafisa mbalimbali wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar watashiriki kwenye hafla ya ufunguzi huo.

Aliongeza kuwa, mafunzo hayo ni kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na Shirika la Marekani linalojihusisha na Masuala ya Utafiti (RTI).

CUF yajikabidhi mikononi mwa CCM,......’Huwezi kumdharau kiongozi wa CCM na Bado ukategemea Kufanya Mkutano wa Hadhara’

$
0
0
Katibu Mkuu mpya wa Chama Cha Wananchi CUF, Khalifa Suleiman Khalifa amesema katika kipindi cha uongozi wake atahitaji kushirikiana kwa karibu na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi ili kutimiza majukumu yake.

Ameyasema hayo jijini Dar es salaam wakati akizungumza na kituo EATV, ambapo amesema katika kuhakikisha CUF mpya inazaliwa atahakikisha anashirikiana na baadhi ya viongozi wenzake wa vyama vya upinzani pamoja na Chama Cha Mapinduzi CCM.

Amesema kuwa akikutana na kiongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) atamwambia kuwa chama ni taasisi ambayo inadhamira ya kujenga nchi, hivyo atamuomba ushirikiano ili kuweza kupata mafanikio ya vyama.

“Ninaposema ushirikiano sisemi mimi nitachukua ilani yao nikaitekeleza, napokutana na Bashiru kwanini nigombane naye nikitengeneza ugomvi na Bashiru nitafaidika nini yeye ni Katibu Mkuu wa Chama Tawala sasa usipozungumza vizuri na viongozi wa CCM, unadhani utafanya mkutano wa hadhara,”amesema Khalifa Suleiman.

Sasa ni Zamu Yeu....Taifa Stars Wamefanikiwa Kufuzu Kwenda Fainali za AFCON2019 Baada ya Kuichapa Uganda Bao 3-0

$
0
0
Timu ya taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' imefanikiwa kuvuka kihunzi cha mwisho katika Uwanja wa Taifa na kufuzu michuano ya mataifa Africa AFCON.

Taifa Stars imeibuka na ushindi wa bao 3-0 dhidi ya timu ya taifa ya Uganda ' The Cranes', bao la kwanza likifungwa na Simon Msuva katika dakika ya 21, Erasto Nyoni dakika ya 51 na Aggrey Morris akimalizia bao la tatu katika dakika ya 57 na kupelekea Tanzania kutimiza ndoto yake ya muda mrefu kushiriki michuano hiyo.

Kwa ushindi huo Taifa Stars inafuzu fainalim za AFCON nchini Misri ikiwa katika nafasi ya pili kwenye kundi L, kwa jumla ya pointi 8, Lesotho ikishuka hadi nafasi ya tatu kwa pointi 6 baada ya kutoka sare ya bila kufungana na Cape Verde ambayo imemaliza mkiani kwa pointi 5.

Ikumbukwe kuwa mara ya mwisho kwa Tanzania kushiriki michuano ya AFCON  ni mwaka 1980 nchini Nigeria, ambapo sasa baada ya kufuzu michuano hiyo, inaungana na Uganda, Kenya na Burundi kwa upande wa nchi za Afrika Mashariki.

Rais Magufuli Aipongeza Taifa Stars Kwa Kufuzu Afcon

$
0
0
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ameipongeza Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) kwa kufuzu kucheza fainali za michuano ya Afrika (AFCON 2019).

Mhe. Rais Magufuli ambaye alikuwa akifuatilia pambano hilo kupitia Luninga amerekodiwa picha ya video akifurahia ushindi baada ya pambano la Taifa Stars na Timu ya Taifa ya Uganda (The Cranes) kumalizika kwa Taifa Stars kupata ushindi wa Magoli 3 kwa 0.

Mhe. Rais Magufuli amesema ushindi huo ni heshima kubwa kwa nchi na amewapongeza wachezaji na Watanzania wote kwa kufanikiwa kupeleka Timu yao ya Taifa katika fainali za AFCON ikiwa ni miaka 39 tangu ilipofanikiwa kufika hatua hiyo mwaka 1980.

Mchezo wa Taifa Stars na The Cranes umefanyika katika uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam leo tarehe 24 Machi, 2019.
Viewing all 45270 articles
Browse latest View live




Latest Images