Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), imebaini dosari katika uwekezaji uliofanywa na Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), katika ununuzi wa ardhi na ujenzi kwenye miradi saba ambayo inaigharimu serikali mabilioni ya shilingi.
Uchambuzi wa kamati hiyo kuhusu miradi hiyo saba, unaonyesha jumla ya Sh. bilioni 27.1 ambazo ni mali ya wanachama wa NSSF, zipo hatarini kupotea kutokana na uamuzi wa uwekezaji usiokuwa na tija.
Miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa Hospitali ya Apollo-Dar es Salaam, ujenzi wa jengo la ubalozi na biashara Nairobi-Kenya, uzalishaji wa umeme Mkuranga na ujenzi wa nyumba katika eneo la Kiseke na Bugarika mkoani Mwanza.
Mingine ni mradi wa Mwandiga Transport Terminal, ununuzi wa ardhi katika mikoa ya Pwani na Dar es Salaam na ujenzi wa nyumba katika kitalu namba 249 kilichopo eneo la Njiro mkoani Arusha.
Akiwasilisha taarifa ya shughuli za kamati hiyo kwa mwaka 2018, Mwenyekiti wa PAC, Naghenjwa Kaboyoka, alisema taarifa ya ukaguzi maalum uliofanyika NSSF, imebainisha udhaifu mkubwa katika suala la uwekezaji.
“Ukaguzi huu maaalum wa miradi ya NSSF ulilenga zaidi miradi inayohusu ununuzi wa ardhi katika maeneo mbalimbali hapa nchini. NSSF iliwekeza miradi kadhaa ya uwekezaji, ambayo kwa kiasi kikubwa haijaleta ufanisi hivyo kuashiria matumizi yasiyofaa ya fedha za umma,” alisema.
Alisema kamati yake imefanya uchambuzi wa kina wa miradi hiyo kama ilivyowasilishwa katika taarifa ya ukaguzi maalum wa NSSF kwa mwaka 2016/2017 na kubaini dosari ambazo zinaweza kuisababishia serikali hasara.
Katika mradi wa ujenzi wa Hospitali ya Apollo ya Dar es Salaam, alisema mkataba wa mradi huo ulisainiwa Septemba 23, 2014 kati ya NSSF na Apollo Hospital Enterprises Limited, Singapore.
Alisema makubaliano ya mradi huo yalikuwa Apollo watoe vifaa na kuendesha hospitali hiyo kwa miaka 15 kwa gharama ambayo ingekubaliwa na kugawanywa asilimia 50 kwa 50 kwa wabia wa mradi huo.
Kwa mujibu wa Kaboyoka, hadi sasa mradi huo umetumia Sh. bilioni 4.19. Hata hivyo, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) alipoutembelea mradi huo Februari 2018, alikuta umetelekezwa na mkandarasi kutokana na eneo hilo kutofikika kwa urahisi kwa sababu ya ujenzi wa mradi wa mabasi yaendayo haraka.
Kwamba hakuna shughuli inayoendelea, hivyo kuthibitisha uwekezaji usio na tija na matumizi yasiyofaa ya fedha za umma.
Kwenye mradi wa ujenzi wa jengo la ubalozi na biashara Nairobi, Kaboyoka alieleza hadi sasa, jumla ya Sh. milioni 854.2 zimekwishatolewa na NSSF katika utekelezaji wa mradi huo. Hata hivyo, kamati inakamilisha taarifa hiyo, hakuna shughuli zozote zinazokuwa zinaendelea katika mradi huo licha ya fedha kutolewa.
Alisema Wizara ya Mambo ya Nje inamiliki sehemu ya ardhi jijini Nairobi na iliingia makubaliano na NSSF kujenga jengo la ubalozi na biashara.
Kaboyoka alisema NSSF walitakiwa kutoa fedha kiasi cha Sh. bilioni 77.4 na Wizara ingechangia ardhi kama sehemu ya mtaji wake.
Kuhusu mradi wa kuzalisha umeme wa Mkuranga (Mkuranga Power Generation), Kaboyoka alisema hadi sasa, NSSF wametumia Sh. bilioni tatu katika mradi huo lakini ukaguzi umebaini ardhi iliyonunuliwa haijawahi kupimwa wala haina mipaka, jambo ambalo litasababisha migogoro siku zijazo.
Alisema: “Pamoja na dosari hiyo, hapakuwapo na upambuzi yakinifu wowote kuonyesha 'economic viability' (faida za kiuchumi) za mradi huo na namna fedha za uwekezaji zitakavyorejeshwa.”
Alisema kuwa kabla ya kuanza kwa mradi huo, NSSF, Shirika la Umeme (Tanesco) na Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC) waliingia makubaliano ya kuanzisha mradi wa kuzalisha umeme katika eneo la Mkuranga mkoani Pwani.
Gharama za mradi huo kwa mujibu wa Kamati ya PAC, zilikadiriwa kuwa dola za Marekani milioni 490. NSSF walinunua ardhi yenye ukubwa wa ekari 100 kwa ajili ya mradi na kuchimba visima 11 vya maji katika eneo hilo.
Kuhusu mradi wa ujenzi wa nyumba katika eneo la Kiseke na Bugarika mkoani Mwanza, Kaboyoka alisema hadi sasa jumla ya Sh. bilioni 1.51 ambazo ni sawa na asilimia 80 ya gharama za mradin zimekwishalipwa.
Alisema ukaguzi umebaini NSSF hawajapewa viwanja vyote kwa mujibu wa mkataba, hivyo kuwapo uwezekano wa kupotea kwa fedha za umma.
Pamoja na dosari hiyo, Kaboyoka alisema uongozi wa Kata ya Buhongwa uliwafahamisha wakaguzi kuwa baadhi ya wanavijiji wa eneo hilo hawakulipwa fidia, hivyo wameamua kuvamia eneo hilo na kusababisha hasara kwa NSSF.
Mradi huo ulianza kutekelezwa mwaka 2008, NSSF wakikubaliana na Halmashauri ya Jiji la Mwanza kununua viwanja 357 katika eneo la Bugarika na viwanja 299 katika eneo la Kiseke kwa gharama ya Sh. bilioni 1.89.
Katika mradi wa ujenzi wa nyumba katika kitalu namba 249 eneo la Njiro jijini Arusha, alisema malipo ya awali yalifanyika Novemba 2010 ni Sh. milioni 132 na malipo ya mwisho yalikuwa Sh. milioni 308 yalifanyika Machi 2011.
“Wakaguzi walipotembelea eneo hilo Januari 2018, walikuta eneo lote limevamiwa na wanakijiji na kujenga majengo kama nyumba za ibada na shughuli nyingine za binadamu. Pamoja na dosari hizo, wakaguzi hawakuweza kupata nyaraka za uhamisho wa ardhi hiyo kutoka kwa muuzaji kwenda NSSF. Hivyo basi, hakuna uwezekano wa fedha za umma zilizotumika kununua ardhi hiyo kurejeshwa tena kwa sasa," Kaboyoka alisema.
Aliongeza kuwa kamati yake imebaini hakuna shughuli inayoendelea katika mradi wa Mwandiga Transport Terminal licha ya kutumika Sh. bilioni 1.85.
Alisema NSSF walipanga kutekeleza mradi wa kituo cha kimataifa cha usafiri katika eneo la Mwandiga, Kigoma lenye ukubwa wa ekari 28 kwa gharama za Sh. bilioni 33.3.
Kaboyoka alisema kuwa hadi sasa, jumla ya ekari 28 za ardhi zimepatikana kwa gharama ya Sh. bilioni 1.85, akihoji ekari moja ya ardhi kununuliwa kwa wastani wa Sh. milioni 66.
Vilevile, alisema wamebaini dosari katika ununuzi wa ardhi mikoa ya Pwani na Dar es Salaam kwa gharama ya Sh. bilioni 15.8.
“Kamati imebaini kuwa ardhi hiyo ilinunuliwa bila ya kuwapo kwa kamati ya uwekezaji ya shirika la (Management Investment Committee - MIC) na haikupata idhini ya bodi. Haikuwa hivyo tu, bali imebaini pia ardhi hiyo haikuwa imepimwa na kufanyiwa tathimini ili kujiridhisha na thamani yake halisi ukilinganisha na bei iliyonunuliwa,” alisema.
Kutokana na uwekezaji huo usiokuwa na tija, Bunge liliazimia serikali ifanye uchunguzi wa wahusika wote waliohusika katika mchakato wa ununuzi wa ardhi husika kwa malengo ya uwekezaji ambao haukuwa na tija na kisha kuchukua hatua stahiki kwa kuzingatia matokeo ya uchunguzi.
Pia, serikali na bodi za mifuko mipya ya hifadhi za jamii iliyoundwa zihakikishe masuala ya uwekezaji yanafanyika kwa kuzingatia sheria na miongozo ya mamlaka husika kama Mamlaka ya Usimamizi wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) na Benki Kuu (BoT) ili kuepuka uwekezaji usiokuwa na tija kwa taifa na kwa wanachama wa mifuko husika.