Kutokana na tukio la bomu lililolipuka katikati ya jiji la Nairobi siku ya Jumamosi usiku, idara ya polisi sasa imewatahadharisha Wakenya kuwa waangalifu wakati huu na kuripoti mtu ama kisa chochote kisicho cha kawaida.
Katika chapisho lake katika mtandao wa Twitter huduma hiyo ya kitaifa ya polisi imewasihi raia kusaidia vikosi vya usalama kukabiliana na tishio lolote kupitia kutoa habari muhimu.
Pia, imewataka Wakenya kuendelea na shughuli zao za kwaida ikisema waathiriwa wawili wa mlipuko huo waliopata majeraha madogo, walipata matibabu na kwenda nyumbani.
Wamesema, polisi imeanza uchunguzi kupitia kutazama picha za kamera za CCTV ili kumnasa mmiliki wa kilipuzi hicho aliyedaiwa kutoroka.
Siku ya Jumamosi usiku shambulio la bomu lilitokea katikati ya jiji la Nairobi na kuwajeruhi watu wawili kulingana na maafisa wa polisi .
Walioshuhudia wanasema kuwa mlio mkubwa ulisikika katika eneo la Odeon, moja ya viunga vyenye shughuli nyingi na mikusanyiko ya watu wengi katikati ya jiji la Nairobi.
Bomu hilo lilikuwa limefichwa ndani ya begi na kusukumwa kwa mkokoteni.
Mkuu wa polisi wa jiji la Nairobi Philip Ndolo aliwaambia wanahabari kuwa, bwana mmoja mwenye asili ya Kisomali alikodi mkokoteni na kupakia begi lake, na walipofika eneo la tukio, kwenye makutano ya barabara za Tom Mboya na Latema mmiliki huyo wa begi alitoweka.
“Alimhadaa mwenye mkokoteni kwa kumwambia amsubiri akafuate kitambulisho chake ambacho alikisahau... hakurudi na baada ya muda mfupi kilipuzi kilichokuwamo ndani ya begi hilo kililipuka,”amesema bwana Ndolo.
Mlipuko huo umewajeruhi mwendesha mkokoteni na mfanyabiashara ndogondogo aliyekuwepo karibu na mkokoteni.
Mlio mkubwa wa bomu hilo ulizua taharuki kubwa kwenye eneo hilo lenye stendi nyingi za mabasi ya abiria.
Shambulio hilo linakuja siku chache toka viunga vya hoteli ya kifahari ya DusitD2 kushambuliwa na kupelekea vifo vya watu 21.
Tayari eneo hilo limefungwa na polisi na vikosi vya kutegua mabomu vimeshawasili eneo la tukio.
Mlipuko huo unajiri huku maafisa wa poliis wakitoa tahadhari ya kiusalama kwa Wakenya