Quantcast
Channel: MPEKUZI
Viewing all 45270 articles
Browse latest View live

Nape Nnauye Atoa Kauli Kuhusu Wabunge na Madiwani Wanaohama Vyama

$
0
0
Mbunge wa Mtama (CCM), Nape Nnauye, amesema ipo haja ya kupitiwa upya kwa sheria inayosimamia thamani ya kura hasa katika kipindi hiki cha wabunge na madiwani kuhama vyama vyao.

Nape amesema kuwa  ni vyema kukawa na sheria ambayo itampa mamlaka mbunge au diwani anayehama chama baada ya uchaguzi, aendelee kuwa na nafasi hizo katika chama anachokwenda ili kuokoa kiasi kikubwa cha fedha kinachotumika katika chaguzi ndogo kwenye maeneo ambayo mbunge au diwani amehamia chama kingine.

Ametoa kauli hiyo akiwa kwenye ofisi ndogo za Bunge visiwani Zanzibar, katika mafunzo ya siku mbili ya kamati ya uongozi, makamu wenyeviti wa kamati za Bunge pamoja na wajumbe wa tume ya utumishi wa Bunge ambapo amesema pamoja na uwepo wa wimbi kubwa la wanasiasa kuhama, wapigakura wanatakiwa kupewa thamani yao kwa kuwa wakati wa uchaguzi wao ndio uhitajika kupiga kura kuchagua wawakilishi wao.

"Siwezi kupingana na Katiba kuhusu hamahama za wanasiasa lakini ni vyema thamani ya wapiga kura ikatambulika vyema, bado thamani ya mpiga kura inapaswa kuenziwa,” amesema Nape.

Wakati hayo yakijiri Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt. Bashiru Ally anatarajiwa kufanya  ziara ya kikazi ya siku nne visiwani humo kuanzia leo  Agosti 17 hadi 20 mwaka huu.

Dk.Bashiru anafanya ziara hiyo kwa mara ya kwanza tangu ateuliwe kushika nafasi hiyo Mei mwaka huu baada ya aliyekuwa Katibu Mkuu Abdulrahman Omar Kinana kustaafu.

Madiwani Wengine Wawili CHADEMA Wajiuzulu na Kuhamia CCM Leo

$
0
0
Madiwani wawili wa Chadema mkoani Kilimanjaro  wamejivua uanachama na kujiunga na CCM.

Waliohama chama hicho leo Agosti 17 ni aliyekuwa diwani wa kata ya Romu wilayani Hai, Shilyimaufoo Kimaro na diwani wa kata ya Vumari, Wilayani Same, John Msofe.

Akizungumzia kuondoka kwa madiwani hao Katibu wa Chadema mkoa wa Kilimanajro,Basil Lema amesema ni kweli madiwani hao wameondoka kwa kile wanachodai wao ni kuunga mkono juhudi za Rais.

Lema amesema kuwa anajua madiwani hao wanahama chama hicho kutokana na baadhi yao kutishiwa uhai na usalama wa maisha yao na wengine wanaondoka kwa sababu ya madeni waliyonayo au maslahi yao binafsi.

“Madiwani wanaobaki wabaki na wale wanaoondoka waondoke lakini tunajua wanaondoka kwa sababu ya vitisho wanavyopata na wengine wanaondoka kutokana na madeni walionayo wakijifanya wanaunga mkono jitihada za Rais,”amesema.

Katibu Mkuu CCM Naye Kajitosa Sakata la Ubalozi wa Marekani Kudai Uchaguzi wa Marudio Haukuwa Huru na wa Haki

$
0
0
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Bashiru Ally, ameitaka Marekani na taasisi za kimataifa kuheshimu uhuru wa Tanzania.

Amesema kauli iliyotolewa na Marekani kuhusu uchaguzi mdogo wa marudio uliofanyika Agosti 12, mwaka huu katika maeneo mbalimbali nchini, inagusa maeneo mengi na ni matarajio yake kwamba taasisi zote za nchi zinazohusika zitazingatia madukuduku yao.

Kauli hiyo ya Dk. Bashiru imekuja siku mbili baada ya Ubalozi wa Marekani kutoa tamko kuhusiana na uchaguzi huo ambapo ilisema uligubikwa na vurugu na pia haukufuata sheria.

“Nimeisoma na nimeielewa, sisi kama chama, tunazingatia zaidi uhuru wa kitaifa kwamba taifa hili ni taifa huru na CCM kina dhamana ya kusimamia uhuru wa kitaifa.

“Ninachojua mimi chaguzi zote zimefanywa kwa msingi wa sheria na matarajio yangu ni kwamba Marekani na taasisi nyingine za kimataifa, zitaheshimu uhuru wa taifa letu,” amesema Dk. Bashiru akihojiwa Kituo cha Deustche Welle cha Ujerumani.

Waziri Mkuu Atoa Maagizo Mazito kwa Wakuu wa Wilaya Nchini

$
0
0
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewaagiza wakuu wa wilaya nchini washirikiane na Madiwani katika halmashauri zao wafanye tathmini ya mali zote zinazomilikwa na halmashauri vikiwemo vibanda vya biashara ili kujiridhisha kama viwango vinavyotozwa vinalingana na hali halisi ya uchumi kwa sasa.

Amesema licha ya tathmini hiyo kuwawezesha kufahamu viwango vinavyotozwa, pia itasaidia halmashauri kubaini watu wa kati ambao wanawatoza wafanyabiashara fedha nyingi na kuilipa halmashauri fedha kiduchu, jambo linalochangia kuikosesha Serikali mapato inayostahili.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Ijumaa, Agosti 17, 2018) wakati akizungumza na watumishi wa halmashauri ya Mji wa Nzega na wa Halmashauri ya wilaya ya Nzega pamoja na Madiwani katika ukumbi wa Halmashauri ya Mji wa Nzega akiwa kwenye ziara yake ya kikazi wilayani Nzega, Tabora.

Ametoa agizo hilo baada ya Mbunge wa Nzega Mjini, Husein Bashe kuomba Serikali iingilie kati mgogoro uliopo baina ya halmashauri na wafanyabiashara kuhusu mradi wa vibanda vya biashara katika eneo la Soko Kuu la Nzega ambavyo vimejengwa na wafanyabiashara katika ardhi ya halmashauri kwa makubaliano ya kulipa kodi.

Uongozi wa halmashauri ya Mji wa Nzega uliamua kupitia upya mkataba wa mradi huo kwa sababu ulikuwa hauinufaishi, hivyo ilianzisha mpango wa maboresho ambapo ilibaini kuwepo kwa watu wa kati waliokuwa wakiwatoza wafanyabiashara zaidi ya sh 150,000 kwa mwenzi na kuilipa halmashauri sh. 30,000 kwa mwezi.

Pia ilibaini kwamba baadhi ya wamiliki wa awali wa vibanda waliviuza kwa wafanyabiashara wengine kwa bei kubwa bila ya kuishirikisha halmashauri na ilivyotaka kuvichukua ili wafanyabiashara waendelee kuwa wapangaji kwa lengo la kuondoa mtu wa kati, ndipo ulipoibuka mgogoro wa umiliki wa vibanda hivyo.

Waziri Mkuu amesema migogoro ya aina hiyo huwa haiishi kwa wakati katika maeneo mengi kwa sababu baadhi ya vibanda hivyo vinamilikiwa na Wakuu wa Idara, Madiwani na baadhi ya watumishi katika hailashauri husika, jambo linalozikosesha halmashauri mapato. “Wakuu wa wilaya shughulikieni hili,”.

Pia, Waziri Mkuu amezishauri halmashauri zinazomiliki vibanda vya biashara hususani kwenye maeneo yenye migogoro watumie leseni za biasahara zinazofanyakazi kwa kuzitambua na kuingia mikataba na wamiliki wake ili kuondoa uwepo wa mtu wa kati.

Kadhalika, Waziri Mkuu amewataka watumishi wa umma wanaomiliki vinanda vya biashara kwenye eneo hilo watoe taarifa za umiliki wao ili kuondoa mgongano wa kimaslahi pindi wanapokuwa kwenye vikao vya kujadili namna bora ya kuipatia ufumbuzi migogoro ya vibanda vya biashara vinavyomilikiwa na halmashauri katika maeneo yao.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewataka viongozi wa halmashauri na wilaya wawahamasishe wananchi kwenye maeneo yao juu ya umuhimu wa kujiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF), hivyo watakuwa wamejihakikishia upatikanaji wa huduma za afya bure kwao na familia zao.

Pia amempongeza Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Bw. Agrey Mwanri kwa jitihada kubwa za kupanua wigo wa kuboresha huduma za afya kupitia CHF, ambapo kwa mkoa huo wanachama wa mfuko huo wanaweza kutibiwa kwenye hospitali zote za Serikali tofauti na maeneo mengine ambayo huduma hiyo inaishia kwenye hospitali za wilaya tu.


IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
IJUMAA, AGOSTI 17, 2018.

Waziri Dk. Kigwangalla kuruhusiwa muda wowote MOI.....Rais Mstaafu Jakaya Kikwete Amtembelea tena

$
0
0
Na Andrew Chale, Dar
Rais Mstaafu wa awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amemtembelea na kumjulia hali Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Dkt. Hamisi Kigwangalla aliyelazwa katika wodi maalum kitengo cha Taasisi ya mifupa MOI,  hospitali ya Taifa Muhimbili jijini Dar es Salaam kwa mara nyingine tena.

Hii inakuwa ni mara ya tatu kwa Kikwete kumtembelea Dk Kigwangalla ambapo awali alimtembelea Agosti 8,2018 alipokuwa amelazwa Wodi ya Mwaisela akipatiwa Matibabu ya awali na juzi Agosti 15,2018 katika wodi ya Taasisi ya Mifupa MOI.

Akiwa hospitaini hapo mapema jana, Kikwete ameweza kumjulia hali na kubadilishana nae mawazo mbalimbali huku akimtakia unafuu  aendelee na majukumu yake ya kila siku na akimpongeza kwa shughuli zake anazozifanya katika kuinua sekta ya Utalii pamoja na kulinda rasilimali za Maliasili.

“Nikutakie kheri. Nashukuru kwa kukuta unaendelea vizuri sasa na nilikuja ukiwa upo unaongea ukiwa umelala kitandani na kwa sasa nimekuja tena umeweza kuimarika na hata kutembea na kukaa kama hivi hongera sana” alieleza Kikwete wakati akimjulia hali Waziri Kigwangalla wodini hapo.

Tayari jopo la Madaktari bingwa wa MOI wamebainisha kuwa Dkt. Kigwangalla kwa sasa anaendelea vizuri na muda wowote anaweza kuruhusiwa kurejea nyumbani ambapo kwa sasa sehemu zilizobakia ni mkono wake wa kushoto ambao kila siku unaendelea kuimarika.

Hata hivyo, Dkt. Kigwangalla amemweleza Kikwete kuwa kwa sasa hali yake inaendelea kuwa vizuri na muda wowote anaweza kuruhusiwa kurejea nyumbani  huku akiendelea na mazoezi kidogokidogo.

Aidha, jioni ya jana Dkt. Kigwangalla ameweza kufanya mazoezi ya kutembea umbali wa zaidi ya kilometa moja kuanzia kwenye viunga vya Hospitali hiyo na kuzunguka maeneo yanayozunguka Muhimbili na baadae kupanda kwa kutumia ngazi katika jengo anapopatiwa matibabu kwa miguu mpaka gorofa ya sita.

Waziri Dkt. Kigwangalla alipata ajali ya gari mnamo Agosti 4, 2018 huko Manyara akiwa katika ziara ya kikazi ambapo katika ajali hiyo iliyokuwa na watu 6, Afisa Habari wa Wizara hiyo Hamza Temba alifariki dunia huku watano wakijeruhiwa akiwemo yeye anaendelea na matibabu Hospitalini hapo.


Watakaohujumu Miundombinu Ya Umeme, Maji Kushtakiwa Kwa Uhujumu Uchumi

$
0
0
Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kwa kushirikiana na Shirika la Umeme (Tanesco), Mamlaka ya Maji na Majitaka Mkoa wa Dar es Salaam (Dawasco) na kampuni za simu, imeanzisha operesheni ya kuwasaka wanaohujumu miundombinu ya kampuni hizo.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa amesema operesheni hiyo imeanzishwa baada ya kuwepo kwa matukio kadhaa ya uhalifu kwa kutumia mitandao na uhujumu wa wa miundombinu ya Dawasco na Tanesco.

“Tumeanzisha operesheni hii maalumu ili kukabiliana na wahujumu uchumi kwa njia ya mitandao na kuharibu miundombinu ya kwa kujiunganishia maji na umeme kinyemela ilihali wakijua ni makosa na wanahatarisha afya zao.

“Watu wasio waaminifu wanatumia mafuta ya transfoma kukaangia chipsi ndiyo maana watu wanaumuka, utakuta mtu shavu la kushoto halilingani na la kulia.

“Wanaojijua wamehujumu miundombinu hiyo  wajisalimishe kabla operesheni haijawafikia, tukiwakamata tutawatia mbaroni kwa kesi ya kuhujumu uchumi wa nchi,” amesema Mambosasa.

Kwa upande wa Mkurugenzi wa Dawasco, Cypriani Luhemeja, amesema kutokana na uhujumu huo mamlaka hiyo inapoteza asilimia 40 maji yanayozalishwa.

“kwa sasa tunazalisha maji ya kutosha na tunatarajia hadi kufikia mwaka 2020 wananchi wote wa Mkoa wa Dar es Salaam watapata maji ya kutosha,” amesema.

Chadema yateua watakao gombea, Ukonga,Korogwe na Monduli

$
0
0
Chama cha Demokrasia na Maendeleo, (CHADEMA), kimetangaza majina ya wagombea wake watakaowania ubunge katika majimbo ya Ukonga, Korogwe Vijijini na Monduli kupitia kikao cha kamati kuu ya chama.

Katibu wa chama hicho kanda ya kaskazini Amani Golugwa amesema kuwa tayari chama hicho kupitia mkutano wake kimekwisha pitisha majina ya watakaopeperusha bendera za chama hicho katika uchaguzi mdogo wa Septemba 16, 2018.

Golugwa amewataja wagombea hao kuwa ni Amina Ally atakayegombea ubunge jimbo la Korogwe Vijijini, aliyekuwa Diwani wa kata ya Lepurko Yonas Masiaya Laizer atasimama jimbo la Monduli pamoja na Asia Msangi atakayeiwakilisha Chadema jimbo la Ukonga jijini Dar es salaam.

Hatua hiyo imechukuliwa baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kutangaza Uchaguzi Mdogo wa Ubunge katika majimbo matatu na wa udiwani katika kata mbili za Tanzania Bara utakaofanyika Septemba 16, mwaka huu.

Uchaguzi huo utafanyika ikiwa ni mwezi mmoja kupita tangu ufanyike uchaguzi mwingine mdogo katika jimbo la Buyungu wilayani Kakonko mkoani Kigoma pamoja na kata 79 nchini ambapo Chama cha Mapinduzi (CCM) kilishinda kwa asilimia 100%.

Marekani yadai China inajiandaa kuishambulia kijeshi

$
0
0
Marekani imedai kuwa vikosi vya China vinafanya mazoezi yenye nia ya kujiandaa kuishambulia Marekani na washirika wake katika Bahari ya Pacific.

Kwa mujibu wa ripoti ya makao makuu ya kijeshi ya Pentagon yaliyoko Washington D.C kwa Bunge la nchi hiyo, China imeongeza uwezo wake wa kutuma ndege za makombora umbali mrefu zaidi.

Imeeleza kuwa China imeendelea kuongeza bajeti yake ya kijeshi hadi $190 bilioni, ikiwa inaanza kuisogelea ile ya Marekani, kwa theluthi.

“Kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita, jeshi la China limeongeza kikosi chake na makombora kupitia njia ya maji, imepata uzoefu zaidi katika mapambano ya eneo la ukanda wa maji na huenda kufanya mazoezi kwa ajili ya mashambulizi dhidi ya Marekani na washirika wake,” imeeleza ripoti hiyo.

Imefafanua kuwa kutokana na maandalizi pia ya makombora ya kutumia ndege za kivita, ni dhahiri kuwa China inaongeza uwezo wake wa kushambulia hadi eneo la Guam na ngome za kijeshi za Marekani za Magharibi mwa Bahari ya Pacific.

Ripoti hiyo pia imedai kuwa China inafanya maandalizi ya kutaka kuiunganisha kijeshi Taiwani na taifa hilo ili kujiongezea nguvu. Imeeleza kuwa inachotaka kufanya ni kuchelewesha uwezekeano wa Marekani kuingilia mpango wake wa kuiunganisha Taiwani.

Hata hivyo, China haijasema lolote kuhusu madai ya Marekani.

Nchi hizo mbili zimekuwa katika mgogoro wa kibiashara katika kipindi cha hivi karibuni.

Mkuu wa Mkoa Paul Makonda alivoshuhudia mfumo wa anwani za makazi na Postcode kutoka TCRA

$
0
0
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Paul Makonda leo amefungua semina ya kimkakati inayolenga kulifanya jiji la Dar es salaam kuwa katika mpangilio wa kisasa na kuhakikisha mitaa yote inawekwa katika mfumo wa anwani za makazi na Postikodi Kama ilivyo kwa majiji makubwa ulimwenguni.

RC Makonda amesema Mfumo huo ni ukombozi mkubwa kwa wananchi kwakuwa utarahisisha huduma kwa wananchi ikiwemo kuwezesha kila mwananchi kuwa na anwani, kuwasaidia wageni kujua maeneo, kudhibiti wezi na matapeli, ulinzi na usalama, kusaidia kampeni ya usafi pamoja na kusaidia Jeshi la zimamoto na uokoaji kufika haraka kwenye eneo lenye dharura Kama ajali ya Moto au nyinginezo na kuokoa maisha.

Aidha RC Makonda amewapongeza Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania TCRA kwa kuzifikia Kata 45 Kati ya 102 za mkoa huo na kueleza kuwa atawapatia ushirikiano wa kutosha kuhakikisha Mfumo wa anwani za makazi na Postikodi unafikia jiji Zima.

Pamoja na hayo RC Makonda amewaomba TCRA kupeleka elimu hiyo kwa Madiwani na wenyeviti wa mitaa ili kuwajengea uelewa.

Mfumo wa Anwani za Makazi na Postikodi unalenga kuhakikika kila Eneo, Kata na Mtaa vinapewa majina na kila nyumba inakuwa na namba ya utambuzi.

Watu Watano Watiwa Mbaroni Kwa Tuhuma za Kugushi Nyaraka na Kujipatia Milioni 284

$
0
0
Watu watano wakiwemo watumishi wanne wa Hazina ndogo Kibaha wanashikiliwa na polisi mkoani Pwani kwa tuhuma za kughushi nyaraka mbalimbali za malipo na kuiba Sh284.8milioni ambazo ni fedha za Serikali.

Watuhumiwa hao wanadaiwa kutenda kosa hilo kati ya Aprili na Mei, 2018, walishirikiana na ofisa mmoja wa Jeshi la Magereza mkoani humo.

Akizungumza leo Ijumaa Agosti 17, 2018 kamanda wa polisi mkoani Pwani, Jonathan Shanna amesema watuhumiwa hao waliiba fedha hizo kwa vielelezo vinazoonyesha zililipwa mzabuni wa kampuni ya Lukozi na Usambara Grocery and Vegetable Supplies ya mkoani humo.

Shanna amewataja watuhumiwa hao Stanley Kansabala, (45), mkazi wa Kigamboni Dar es salaam, Boaz Lyimo (31), mkazi wa Kimara, Imani Kilembe (43), mkazi wa Suka ambaye yeye katika upekuzi anadaiwa kukutwa na Sh4.6milioni nyumbani kwake na Hallo Ntambi (38) aliyekutwa na Sh 4.2milioni nyumbani kwake, wote wakiwa ni wahasibu wa Hazina ndogo.

Mwingine ni ofisa wa Jeshi la Magereza mkoani hapa anayeshughulika na kazi za uhasibu SP Komango Makala (53)  mkazi wa Magereza Kibaha na wote watafikishwa mahakamani wakati wowote uchunguzi utakapokamilika.

Amesema pia wamemnasa mkurugenzi wa kampuni hiyo ya Lukola na Usambara, Omary Singano kwa mahojiano zaidi kwa kuwa kampuni hiyo ndiyo imeingiziwa fedha hizo, hivyo amemtaka kutii sheria bila shuruti kwa kufika ofisi ya mkuu wa upelelezi Pwani mara moja.

Katika tukio jingine , hakimu wa mahakama ya wilaya ya Bagamoyo ambaye jina lake linahifadhiwa amekamatwa kwa tuhuma za kushirikiana na matapeli wauzaji wa viwanja  na mashamba kusaini hati mbalimbali katika tarehe tofauti kisha kijipatia Sh18 milioni kutoka kwa ofisa wa Jeshi la Wananchi (JWTZ) kwa njia ya utapeli.

“Hakimu huyu amekuwa akisaini hati mbalimbali zinazotumiwa na matapeli kujiingizia kipato kwa kuwauzia watu eneo moja la ardhi kwa mara mbili,” amesema.

“Anawagongea muhuri wa Serikali anaweka sahihi yake kuwezesha utapeli huu na katika uthibitisho amesaini hati moja ya umiliki ya nyumba na kujipatia Sh18milioni kutoka kwa afisa wa JWTZ.”

Madiwa Wanne CHADEMA Wapigwa 'Stop' Kuhudhuria Vikao Hadi June 2019

$
0
0
Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya siha, limewasimamisha madiwani wanne wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kuhudhuria vikao vya baraza hilo hadi Juni mwaka 2019.

Madiwani hao wanadaiwa kuvunja kanuni ya 10 (d), kwa kuvua joho ambalo ni vazi maalumu lililochaguliwa na madiwani wa halmashauri hiyo kwa ajili ya mikutano ya baraza na hata walipotakiwa na mwenyekiti kuvaa joho hilo wanadaiwa kukaidi.

Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya hiyo, Valerian Juwal, amesema uamuzi huo una baraka za wajumbe wa baraza hilo.

Baadhi ya madiwani wanaodaiwa kusimamishwa ni pamoja na Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Frank Tarimo, Diwani wa Kata ya Ivaeny, Elia Kiwia, Diwani wa Kata ya Kirua, Robert Mrisho na Diwani wa Viti Maalumu Witness Riwa.

Jeshi La Polisi Latahadharisha Wananchi Kuhusu Wamatapeli Wanaotangaza Ajira Za Polisi

Habari Zilizopo Katika Magazeti ya Leo Jumamosi ya Agosti 18

Kwa mara ya kwanza Davido asafiri na ndege yake binafsi

$
0
0
Msanii wa muziki kutokea nchini Nigeria, Davido mara baada ya kuweka wazi kuwa amenunua ndege binafsi, sasa ameanza kupaa nayo.

August 17, 2018, Davido aliingia katika vitabu vya kumbukumbu kuanza kutumia ndege hiyo kwa mara ya kwanza.

Davido ameipa ndege hiyo jina la OBO - Omo Baba Olowo (Maana yake ni Mtoto wa Tajiri) unaweza kuiita kuwa ndege ya mtoto wa tajiri, ilipaa Davido akiwa na mpenzi wake kuelekea Cotonu.

Kwa mara ya kwanza Diamond afunguka kuhusu kuvaa kikuku

$
0
0
Msanii wa Bongo Fleva, Diamond Platnumz kwa mara ya kwanza amejibu sakata la kuvaa cheni za miguuni almaarufu kama Kikuku ambapo amesema  kuwa kitendo hicho kinatafsiri mbali mbali kulingana na nchi husika.

Diamond kupitia Wasafi TV amesema kuwa kwa Marekani au nchini nyingine mtu kuvaa cheni mguuni anaonekana kama shujaa ambaye ametoroka jela.

"Kila nchi ina tamaduni zake na kila nchi ina tafsiri yake. Ukivaa cheni ya mguu kwa ambao wamekaa jela, ukiwa na kesi kubwa unafungwa cheni miguu yote miwli, kwa tafsiri yake ni mtu aliyefungwa jela halafu akatoroka," Diamond ameiambia Wasafi TV.

"Lakini kwenye nchi nyingine unatafsiri vitu vingine, kwa hiyo anayetafsiri ndiye anakosea, anayekifanya hakosei. Naamini mtu hawezi kunipangia nivae kitu gani, atapoteza muda wake, kila mtu na fashion yake na haiwezi kukutafsiri wewe ni mtu wa namna gani," amesisitiza zaidi.

Utakumbuka msanii mkongwe, Dudu Baya alijitokeza na kupinga vikali kitendo cha Diamond Platnumz kuvaa kikuku kwa kueleza kuwa muimbaji huyo anaharibu muziki wa Bongo Fleva.

Hali ya Bobi Wine ni mbaya, hawezi kuongea wala kusimama.,...Bado Anashikiliwa na Polisi

$
0
0
Wanasheria wawili wa msanii wa muziki ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Kyadondo Mashariki Robert Kyagulanyi maarufu Bobi Wine, wamesema mwanasiasa huyo ana hali mbaya kiafya kwani hawezi kutembea wala kuzungumza.

Wakiwa pamoja na familia ya Bobi, awali wanasheria hao walizuiwa kumwona mbunge huyo aliyekamatwa Jumatatu mjini Arua pamoja na wanasiasa kadhaa wa upinzani. Alifikishwa katika Mahakama ya Kijeshi mjini Gulu ambako alishtakiwa Alhamisi kwa kosa la kumiliki isivyohalali bunduki na risasi.Lakini pia ushiriki wake kwenye machafuko katika eneo la Arua, yaliyochangia kushambuliwa kwa msafara wa magari ya rais Yoweri Museveni.

Hata hivyo, alishtakiwa mbele ya wanasheria wake wawili; Asuman Basalirwa (Mbunge wa Manispaa ya Bugiri) na Medard Seggona (Mbunge wa Busiro Mashariki).

Kwa mujibu wa Basalirwa, ambaye alikuwemo kwenye chumba cha mahakama, uso wa mteja wake ulikuwa umevimba na hakuwa anaweza kutembea wala kuongea. Seggona alisema Bobi Wine hakuweza hata kuandikisha maelezo kwa sababu alikuwa katika hali mbaya na alikuwa amefungwa pingu.

“Hali ya Kyagulanyi ni mbaya sana. Ana maumivu makali. Hawezi kuzungumza, na anapata shida sana hata kukaa. Uso wake umevimba na hawezi kuona kwa sababu ya mateso aliyopata kutoka kwa askari wa SFC. Hakuweza hata kuzungumza wakati akisomewa mashtaka na naamini hakuwa anajua kinachoendelea wala kuelewa mashtaka aliyosomewa,” alisema Seggona alipozungumza na wanahabari.

Familia yake haikuruhusiwa kuingia kwenye chumba cha mahakama kusikiliza kesi hiyo chini ya mwenyekiti Luteni Jenerali Andrew Gutti.

Barbara Itungo maarufu kama Barbie, ambaye ni mke wa Bobi Wine alianguka na kuangua kilio wakati wanasheria wa mumewe wakielezea namna alivyoteswa.

“Nikiwa mke na mama, uvumilivu wangu uko majaribuni. Serikali iniruhusu nimwone mume wangu. Nina wasiwasi na hali yake kwa sababu najua alipigwa sana na wanajeshi,” alisema huku akitokwa machozi

Waziri Mkuu: Watendaji Wa Halmashauri Hamuendi Kwa Wananchi........Asema Wingi Wa Mabango Kwenye Mikutano Ya Viongozi Ni Ishara Tosha

$
0
0
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema kuwepo kwa mabango mengi kwenye mikutano ya hadhara  ya viongozi wakuu kunadhihirisha wazi kwamba watendaji wa  Halmashauri hawawatembelei  wananchi katika maeneo yao na kutatua kero mbalimbali zinazowakabili.

“Watendaji hamuendi kuwatembelea wananchi na kusikiliza matatizo yao, haiwezekana wawe wanawasubiri viongozi wa juu na kuwasilisha kero zao, sasa jipangeni haya mabango yote mtakuja kuyajibu kwa sababu hoja zote ni za ngazi ya halmashauri,” alisema.

Aliyasema hayo jana jioni (Ijumaa, Agosti 17, 2018) wakati akizungumza na wananchi wa jimbo la Nzega Mjini kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Parking, ambapo aliwataka viongozi wa halmashauri hiyo kutenga siku maalumu kwa ajili ya kwenda vijijini kusikiliza kero za wananchi na kuzipatia ufumbuzi.

Waziri Mkuu alisema Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli imeelekeza nguvu kubwa katika kuwatumikia wananchi na kutatua kero zao, hivyo itasimamia kuhakikisha kila mtumishi anawajibika kwa kiwango kinachostahili.

Alisema Serikali inataka kuona wananchi wakihudumiwa, Makatibu Tawala wa Wilaya wanatakiwa kujiridhisha kwenye halmashauri zao kama watumishi wa umma wanafanyakazi ipasavyo  na iwapo hawaridhishwi wanatakiwa kutoa taarifa kwenye ngazi husika.

“Serikali hii haimlindi mfanyakazi ambaye ni mbadhilifu, mwizi na ambaye hafanyi kazi kwa weledi au anayebagua wananchi eti kwa uwezo wake wa kifedha au rangi au dini yake au chama chake. Hivi vitu havipo katika Serikali kila mwananchi aliyeko Nzega anatakiwa kuhudumiwa,”alisisitiza

Kadhalika, Waziri Mkuu aliwaagiza Wakuu wa Wilaya na Makatibu Tawala wa Wilaya wafuatilie na kujua kiasi cha fedha kinachopelekwa na Serikali katika halmashauri zao kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ili kujiridhisha kama zinatumika kama ilivyokusudiwa.

“Ni lazima viongozi hao wajue fedha za miradi zilizopatikana katika halmashauri zao ili waweze kwenda kukagua utekelezwaji wa miradi husika na kujiridhisha kama inakidhi viwango na inalingana na kiasi cha fedha kilichotumika,” alisisitiza.

Katika hatua nyingine,Waziri Mkuu alitoa siku 30 kwa  uongozi wa halmashauri ya wilaya ya Nzega uwe umekamilisha ujenzi wa vyumba vya maabara katika shule ya sekondari ya Magengati. Miaka minne iliyopita wananchi walijitolea kwa kujenga maboma na kuiachia halmashauri imalizie hatua zilizofuata.

Waziri Mkuu alitoa agizo hilo wakati akizungumza na wananchi wa jimbo la Nzega Vijijini katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye kijiji cha Usagali, ambapo alisema ni lazima ujenzi wa vyumba hivyo vya maabara ukamilike. “Haiwezekani miaka minne vyumba hivyo viwe havijakamilika,”.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAMOSI, AGOSTI 18, 2018.

Serikali Yapiga Marufuku Saruji Kuuzwa Nje ya Nchi

$
0
0
Katika hatua ya kukabiliana na uhaba wa saruji nchini, serikali imezuia usafirishaji wa bidhaa hiyo na makaa ya mawe kwenda nje ya nchi kabla ya kutosheleza kwanza soko la ndani ya nchi.

Hatua hiyo imefikiwa ili kuwezesha saruji inayozalishwa nchini kuwanufaisha kwanza watanzania na kuwezesha utekelezaji wa miradi mikubwa ya ujenzi inayoendelea hivi sasa. 

Pia serikali imeahidi kuboresha miundombinu ya kwenda na kutoka kwenye viwanda vya kuzalishia saruji na makaa ya mawe ili bidhaa hizo zisafirishwe kwa haraka na ufanisi kwenda sokoni. 

Hatua hiyo inakuja wakati takribani wiki mbili sasa kumekuwa na uhaba wa saruji nchini hatua iliyosababisha ongezeko la juu la bei ya bidhaa hiyo huku maeneo mengine ikikosekana kabisa.

Ili kuweza kupata ufumbuzi wa kudumu wa sakata hilo, juzi Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Stella Manyanya alifanya mkutano na wazalishaji, wasambazaji, wasafirishaji wa saruji na kampuni zinazozalisha makaa ya mawe. 

Kikao hicho kilichodumu kwa takribani saa tatu kilianza saa moja jioni na kumalizika saa nne usiku, huku Naibu Waziri Manyanya akianza kwa kuwataka wadau hao kulipatia uzito unaostahili jambo hilo kwa kuwa linagusa maslahi ya kitaifa huku akiwasihi kutofanya nalo mzaha.

Aliwatahadharisha kuwa jambo hilo linaweza kuwa na uamuzi mzito au wa kawaida na baadaye alianza kusikiliza maoni ya wazalishaji wa saruji kabla ya kuja kwa wadau wengine. 

Baada ya kikao hicho kumalizika, Waziri Manyanya alisoma makubaliano waliyofikia ambapo alisema kwa kuwa kwenye mazungumzo hayo imebainika kuwa kuna kiwango cha saruji ambacho pia huuzwa nje ya nchi, hivyo wamekubaliana kwanza saruji itosheleze soko la ndani kabla ya kuanza kuuzwa nje, vivyo hivyo kwa makaa ya mawe.

 Alisema: ”Ili kuhakikisha soko la ndani linajitosheleza kwanza wanatakiwa kuuza kiwango kikubwa ndani ya nchi na kinachobakia ndio iwe nje na hii haimaanishi kuwa hatutaki wauze nje, hapana ila tunachotaka ni kwanza soko la ndani watanzania na miradi mingine ya ujenzi inufaike”.

Aliongeza: ”Ubovu wa miundombinu ya barabara kwenda na kutoka kwenye viwanda vya kuzalishia makaa ya mawe kumesababisha magari kuchukua muda mrefu zaidi kubeba bidhaa hizo na hivyo kuleta uhaba kwa wazalishaji na hivyo wamekubaliana na Wakala Barabara Tanzania”. 

Alisema, wiki moja kuanzia sasa kutakuwa na kiwango kikubwa cha saruji mitaani na kuwa kila mdau amekubali kutekeleza walichokubaliana huku akiwataka kutambua kuwa saruji ina mchango mkubwa kwa sasa katika kuelekea kwenye Tanzania ya viwanda hasa kutokana na miradi mikubwa inayoendelea kutekelezwa yenye kuhitaji zaidi bidhaa hiyo.

Credit: Habari Leo

ATCL Kuanza Kupasua Anga la Entebe Uganda na Bujumbura

$
0
0
Shirika  la Ndege nchini (ATCL) litaanza kufanya safari za kwenda Entebbe, Uganda na Bujumbura, Burundi kuanzia mwishoni mwa mwezi huu. Kuanza kwa safari hizo ni jitihada za shirika hilo kujitanua kibiashara baada ya kuendelea kufanya vyema katika soko la ndani.

Ndege zitakazofanya safari hizo ni Bombardier Dash 8 Q400 zenye uwezo wa kubeba abiria 76 kila moja. 

Mkurugenzi Mtendaji na Mtendaji Mkuu wa ATCL, Ladislaus Matindi, amesema kuwa safari ya kwenda Entebbe zitaanza Agosti 26, wakati safari za kwenda Bujumbura zitaanza Agosti 30, mwaka huu.

Akifafanua zaidi kuhusu safari hizo, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa ATCL, Josephat Kagirwa, alisema kuwa safari hizo zitakuwa zikifanyika mara tatu kwa wiki. 

Kwa mujibu wa Kagirwa, safari za kutoka Dar es Salaam kupitia Kilimanjaro kwenda Entebbe zitakuwa zikifanyika siku za Jumanne, Ijumaa na Jumapili, wakati safari za kutoka Dar es Salaam kupitia Kigoma kwenda Bujumbura zitakuwa zikifanyika siku za Jumatatu, Jumatano na Jumapili.

“Ndege zote mbili zitakuwa zikianza safari zake kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Dar es Salaam saa 3:30 asubuhi, lakini ndege inayoenda Entebbe itakuwa ikirejea Dar es Salaam saa 8:50 mchana na ile inayoenda Bujumbura itakuwa ikirejea Dar es Salaam saa 10 jioni,”alieleza Kagirwa. 

Kagirwa aliongeza kuwa kwenye kila ndege kutakuwa na daraja la biashara na daraja la kawaida ambapo kwenye daraja la biashara kutakuwa na viti sita na viti vingine 70 vilivyosalia ni kwa ajili ya daraja la kawaida.

Alisema kuwa ATCL imeweka bei nafuu kwa wateja wao watakaokuwa wakisafiri na ndege hizo kwenda Entebbe na Bujumbura, lakini pia utaratibu wa kupata tiketi ni ule ule wa ama kufika kwenye ofisi za ATCL, kukata kwa njia ya mtandao au kupitia kwa mawakala wao. 

Kwa mujibu wa Kagirwa, pamoja na kutoa huduma, lakini lengo za kuanzishwa kwa safari hizo ni kukuza biashara na utalii nchini.

7 Watiwa Mbaroni Kwa Kukutwa na Zana za Kutengeneza Noti Bandia

$
0
0
Jeshi la Polisi mkoani Tabora linawashikilia watu saba kwa tuhuma za kukutwa na zana mbalimbali za kutengeneza noti bandia kwa lengo la kujipatia kipato kwa utapeli. 

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Emmanuel Nley alisema watuhumiwa hao walikamatwa Agosti 8, mwaka huu wakati askari wakiwa katika doria.

Aliwataja waliokamatwa kuwa ni Beatus Taita (28) mkazi wa Mwanza, Pasifili Masawe (33), mkazi wa Ipuli, Shaban Mrisho (26) mkazi wa Mwinyi na Anicet Joseph (27) mkazi wa Uzunguni. 

Wengine ni Hance Mkonongo (31) mkazi wa Block T Mbeya, Denis Simbee (39) mkazi wa Tunduma na Nickson Shitindi (38) mkazi wa Mbozi, Songwe. 

Alieleza kuwa watuhumiwa hao walikamatwa wakiwa na makaratasi yanayotumika kutengeneza noti hizo bandia. Alisema katika mahojiano, watuhumiwa hao walikiri kujihusisha na uhalifu huo.

Katika msako mwingine uliofanyika saa 2.30 usiku siku hiyo polisi walifanikiwa kuwanasa watuhumiwa 12 wa dawa za kulevya katika eneo la Vatican, Kata ya Gongoni Manispaa ya Tabora wakiwa na dawa za kulevya zinazodhaniwa kuwa ni kokeni. 

Waliokamatwa ni Khadja Halfan (40), mkazi wa Isevya, Haji Abdallah (45), mkazi wa Isevya, Ally Sunga (23), mkazi wa mkoani, Elias Msuya (29) mkazi wa Ipuli na Yusuph Sijamini (33), mkazi wa Kalunde. 

Wengine ni Rashid Mrisho (35), mkazi wa Isevya, Rashid Lungwa (37), mkazi wa Isevya, Gumsan Kairo (28), mkazi wa Isevya, Kulwa Chambi (35), mkazi wa Isevya, Mashaka Akida (25), mkazi wa Isevya, Said Salum (25), mkazi wa Chemchem na Miraji Omar (22), mkazi wa Ipuli. 

Alieleza kuwa watuhumiwa wote watafikishwa mahakamani mara moja baada ya upelelezi kukamilika.
Viewing all 45270 articles
Browse latest View live




Latest Images