Quantcast
Channel: MPEKUZI
Viewing all 45270 articles
Browse latest View live

Waziri Kairuki ataka Bilioni 30 sekta ya madini, mafuta zichunguzwe zilipo

0
0
Na Greyson Mwase, Dar es Salaam
Leo tarehe 30 Aprili, 2018 Waziri wa Madini, Angellah Kairuki amezindua ripoti ya Nane ya ulinganishi wa mapato ya Serikali na malipo ya kampuni za madini, mafuta na gesi asilia kwa mwaka wa fedha 2015/16 iliyoandaliwa chini ya Mpango wa Uhamasishaji Uwazi katika Mapato ya Madini, Gesi Asilia na Mafuta Tanzania (TEITI) kwa  kushirikiana na Mtaalam Mwelekezi, Boas & Associates na MM Attoneys.

Akizungumza katika uzinduzi wa ripoti hiyo uliofanyika jijini Dar es Salaam na kukutanisha  wawakilishi kutoka Kamati ya TEITI, Wizara ya Madini, makampuni ya mafuta na gesi, Waziri Kairuki amepongeza  Kamati ya TEITI na Sekretarieti kwa mchango wake katika uandaaji wa ripoti hiyo.

Mbali na  Pongezi hizo, Kairuki ameiagiza Kamati ya  TEITI kuongeza nguvu katika kuhakikisha wananchi wanakuwa na uelewa mpana wa umuhimu na wajibu  wa TEITI kwa kutumia mbinu mbalimbali ikiwa ni pamoja na warsha mbalimbali pamoja na vipindi vya redio na  televisheni.

Amesisitiza kuwa,  kipaumbele kiwekwe kwenye maeneo  yaliyozungukwa na shughuli za utafutaji na uzalishaji wa madini, mafuta na gesi asilia na kupata taarifa ndani ya kipindi cha miezi sita.

Awali akielezea ripoti hiyo,  Kairuki amesema kuwa ripoti hiyo  inahusu tathmini ya mapato ya madini katika kipindi cha kuanzia tarehe 1 Julai, 2015 hadi tarehe 30 Juni, 2016 na kufafanua kuwa jumla ya shilingi 434,627,874,380 zilipokelewa serikalini  kutoka kwenye kampuni 55 za madini, mafuta na gesi asilia zilizoshiriki zoezi la ulinganishi.

Hata hiyo amesema taarifa inaonesha kuwa kampuni zililipa kiasi cha shilingi 465,164,747,725 za kitanzania serikalini na kusababisha tofauti kati ya malipo kuwa ni pungufu ya shilingi 30,536,873,345 za kitanzania chini ya kiasi ambacho Serikali imekiri kupokea.

“ Ni lazima tufahamu ni vipi imejitokeza tofauti hii na ninachukua fursa hii kuelekeza taarifa hii kupelekwa kwa Mkaguzi Mkuu  wa Hesabu za Serikali kwa ajiili ya uchunguzi kama kifungu 18(1) cha Sheria ya TEITI ya mwaka 2015 kinavyotaka,” alisema Waziri Kairuki.

Katika hatua nyingine,  Waziri Kairuki amefafanua kuwa ripoti  imeonesha kuwa sekta ya madini imechangia zaidi kwa asilimia 85 na sekta  ya mafuta na gesi ikionyesha kuchangia asilimia 15 ya mapato ya Serikali chini ya Sekta ya Madini kwa mwaka 2015/16

Akielezea mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Tano katika sekta ya madini, Kairuki amesema kuwa ili kuhakikisha madini yanakuwa na mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi, Serikali imeanza kuchukua hatua kadhaa ikiwa ni pamoja na kufanya mabadiliko ya Sheria ya Madini pamoja na kanuni zake.

Ametaja hatua nyingine ambayo ni endelevu kuwa ni kufanya tathmini ya jinsi gani nchi  inapata mapato yake kwenye sekta ya madini kutokana na hatua mbalimbali zinazochukuliwa.

Ameendelea kusema kuwa jukumu linafanywa na taasisi mbalimbali  za Serikali lakini TEITI nayo inatekeleza jukumu husika kwa kuhakikisha taarifa za mapato ya madini zinatolewa kwa uwazi kwa wananchi na wadau mbalimbali katika Serikali,  Sekta Binafsi na Mashirika yasiyo ya Kiserikali.

Wakati huo huo akizungumza na waandishi wa habari, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila amesema kuwa mara baada ya ripoti kuzinduliwa na kukabidhiwa kwa Kamati ya TEITI hatua inayofuatia ni kamati ya TEITI kuwasilisha ripoti hiyo kwa Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ili achukue hatua kwenye hoja zilizotokana na ripoti hiyo.

Profesa Msanjila amezitaka kampuni nyingine ambazo hazikushiriki katika kipindi cha ukaguzi kujitokeza katika ukaguzi unaofuata ili  takwimu halisi za mapato zifahamike.

Aidha, ametumia fursa hiyo kukaribisha kampuni nyingine zenye nia ya kuwekeza kwenye sekta ya madini kujitokeza kwa wingi  ili sekta ya madini iwe na mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi.

Kamati ya Bunge yaipinga serikali kuhamisha walimu

0
0
Kamati ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii imekosoa utaratibu wa Serikali kuhamisha baadhi ya walimu wa shule za sekondari kufundisha shule za msingi kwa maelezo kuwa kila ngazi ya ualimu ina miongozo na mafunzo yake mahsusi.

Akiwasilisha maoni ya kamati hiyo kuhusu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia mwaka 2018/19 kwa niaba ya mwenyekiti, Peter Serukamba, mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe amesema Serikali inatakiwa kuliangalia suala hilo kwa jicho la pekee.

“Kamati inatambua na kuelewa tatizo la ukosefu wa walimu hasa katika shule za msingi hapa nchini, ila kuchukua walimu wa sekondari kwenda kufundisha shule za msingi si sawa,” amesema Bashe.

Mbunge huyo ameyasema hayo leo Aprili 30 bungeni mjini Dodoma.

“Kumchukua mwalimu wa sekondari kwenda kufundisha shule ya msingi kumepokelewa kwa hisia tofauti miongoni mwa jamii na walimu wenyewe ikiwemo kuhisi kuadhibiwa hivyo kushusha morali ya kufanya kazi.”

Amesema Serikali inapaswa kutazama uamuzi huo kwa jicho la pekee na kufanya uamuzi ulio sahihi kwa mustakabali mzuri wa elimu nchini.

Pia, amesema kamati hiyo ina taarifa kuwa mahitaji ya walimu kwa shule za msingi ni 273,454 lakini walimu waliopo ni 175,946 na hivyo kuwa na upungufu wa walimu 97,508 sawa na asilimia 35.

“Kwa shule za sekondari hasa masomo ya sayansi, mahitaji ni walimu 35,136 lakini waliopo ni 19,285 na hivyo kuwa na upungufu wa walimu 15,851 sawa na asilimia 45.1,” amesema Bashe.

pika amtaka Waziri Mpango kukutana na Waziri wa Nishati ujadili kusuasua kwa miradi wa REA

0
0
Spika wa Bunge, Job Ndugai amemtaka Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango kukutana na Wizara ya Nishati ili kujadili kusuasua kwa miradi wa Wakala wa Umeme Vijijini (Rea).

Ndugai ametoa kauli hiyo leo Aprili 30, 2018 baada ya kumalizika kwa kipindi cha maswali na majibu bungeni mjini Dodoma kutokana na wabunge wengi kusimama na kutaka kuuliza maswali ya nyongeza, zaidi katika maswali yanayohusu wizara hiyo, wakigusia zaidi kukwama kwa miradi ya umeme vijijini.

“Miradi ya Rea imesimama maana kuna wakandarasi wapo lakini mambo hayaendi, miradi hiyo ndio mkombozi wa Watanzania. Waziri wa Fedha hebu kaa karibu na Wizara ya Nishati katika hili,” amesema Ndugai.

Mbunge Awavaa Walimu Wanaofelisha Wanafunzi kwa Rushwa ya Ngono

0
0
Mbunge wa Ulanga Goodluck Mlinga amelitaarifu bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, juu ya vitendo vinavyofanywa na baadhi ya walimu wa vyuo vikuu hapa nchini, vya kufelisha wanafunzi wa kike kwa makusudi.

Akichangia hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Elimu na , Goodluck Mlinga amesema walimu hao ambao wanajifanya ni vidume vya mbegu, hufelisha wanafunzi wa kike ili wawape rushwa ya ngono, kuweza kuwawekea maksi za ufaulu.

“Kumekuwa na tatizo la vyo vikuu, wanafunzi wetu wa kike wanapata shida mno, katika vyuo vyetu vikuu kuna walimu wanajulikana kabisa kuwa hawa walimu ni madume ya mbegu, wanafelisha wanafunzi wa kike, wanataka wawape rushwa za mapenzi ndio wawafaulishe”, amesema Goodluck Mlinga

Pia Mheshimiwa Mlinga amesema yupo tayari kupeleka majina ya walimu hao ambao wapo vyuo vyote nchini kwa Waziri wa Elimu, ili waweze kuchukuliwa hatua stahiki.

“Mheshimiwa Waziri nitashirikiana na wewe kama utapenda unipe ushirikiano, nitakuletea majina ya vyuo vikuu vyote Tanzania, ya walimu ambao madume ya mbegu kazi yao ni kufelisha wanafunzi na kutaka rushwa za ngono”, amesema Mheshimiwa Mlinga.

Habari Zilizopo Katika Magazeti ya Leo Jumanne ya May 1

Sakata la Nondo kusimamishwa masomo UDSM laibuka bungeni

0
0
Mbunge wa Mchinga (CUF), Hamidu Bobali amesema uamuzi wa Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM) kumsimamisha masomo mwanafunzi wake wa mwaka wa tatu, Abdul Nondo unakitia aibu chuo hicho na ni kinyume na haki za binadamu.

Akizungumza jana Jumatatu Aprili 30, 2018 wakati wa mjadala wa bajeti ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia mwaka 2018/19, Bobali alisema sheria iliyotumika kumsimamisha masomo inatakiwa kufutwa.

“Hivi ni wanafunzi wangapi ambao wameshtakiwa na kesi zao zipo mahakamani lakini wanaendelea na masomo. Hili suala la Nondo linakitia aibu chuo pengine watueleze tu kwamba jambo hili ni la kisiasa,” alisema Bobali.

Wakati Bobali akitoa maelezo hayo, mbunge wa Magogoni (CUF), Dk Ally Yusuf Suleiman aliomba taarifa kwa Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge na kubainisha kuwa hata wabunge wapo walioshtakiwa, wengine kufungwa lakini mpaka sasa bado wanaendelea na ubunge wao.

“Napenda kumpa taarifa mzungumzaji (Bobali) kuwa hata wabunge wapo walioshtakiwa lakini mpaka kufungwa lakini bado ni wabunge hadi sasa,”alisema Suleiman.

Nondo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi Tanzania (TSNP) amesimamishwa masomo kuanzia Machi 26, 2018 kwa barua iliyoandikwa na Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa William Anangisye, aliyeeleza kuwa amesimamishwa kwa mujibu wa taratibu za chuo hicho.

Nondo alijikuta kwenye misukosuko na vyombo vya dola tangu alipotoweka katika kile kilichoelezwa kuwa ni katika mazingira ya kutatanisha Machi 6 na kuonekana Machi 7 wilayani Mufindi, Iringa.

Margaret Sitta ataka kuwe na chombo huru kusimamia elimu

0
0
Mbunge wa Urambo (CCM), Margaret Sitta ameishauri Serikali kuunda chombo huru cha kusimamia elimu nchini ili kuondoa utaratibu uliopo sasa ambapo Serikali ndio msimamizi wa shule zake na shule binafsi.

Akizungumza jana Aprili 30, 2018 wakati akichangia mjadala wa Bajeti ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia mwaka 2018/19, Margaret ambaye alikuwa waziri wa wizara hiyo kwa kipindi cha miaka miwili na nusu katika Serikali ya Awamu ya Nne, amesema chombo hicho kitasaidia kuweka usawa katika elimu.

“Lazima kuwe na chombo maalum cha kusimamia elimu kwa kuchambua sera, lugha za kufundishia kama ni sahihi ama si sahihi, kusimamia mitihani inayotungwa je iendelee kama ilivyo na kutazama mazingira ya shule,” alisema Margaret.

Bajeti ya wizara hiyo ya Sh1.4trilioni imewasilishwa jana asubuhi, wabunge wengi walioijadili waligusia kuanzishwa kwa chombo hicho, baadhi wakibainisha kuwa Serikali imekuwa ikizikandamiza shule binafsi badala ya kuziboresha wakati ikijulikana wazi kuwa shule hizo kwa sasa zinafanya vizuri zaidi kuliko za Serikali.

Margaret pia ameitaka Serikali kuanzisha vyuo zaidi vya maendeleo na ufundi ili vijana zaidi waweze kupata elimu na kujiajiri.

Live Kutoka Iringa: Maadhimisho Ya Sherehe Za Mei Mosi 2018

0
0
Live Kutoka Samora Iringa: Maadhimisho Ya Sherehe Za Mei Mosi

Peter Msigwa amkaribisha Rais Magufuli Iringa....Awataka Wafuasi wa CHADEMA Wasivae Sare Zao

0
0
Mbunge wa Iringa Mjini kupitia tiketi ya CHADEMA, Mhe. Peter Msigwa amewakaribisha wageni wote mkoani humo akiwemo Rais Magufuli katika kusherehekea siku ya Mei Mosi na kuwaomba wanachama wa CHADEMA na wafuasi wa UKAWA wasivae jezi za vyama kwenye sherehe hizo.

Mchungaji Msigwa kupitia taarifa aliyoitoa kwa vyombo vya habari leo Mei 1, 2018 amesema kuwa viongozi wa  Chama Cha Mapinduzi (CCM) wanaichukulia siku ya wafanyakazi duniani kama sehemu ya kufanya siasa kwenye majukwaa, kitu ambacho kimepelekea bendera za CHADEMA kung’olewa kwenye nguzo na kuwekwa bendera za CCM.

“Wenzetu wanatumia sherehe hizi kisiasa kwa kung’oa bendera za chadema na kuweka bendera za CCM hata kwenye nguzo za umeme! Kinyume cha utaratibu, Utadhani ni sherehe ya kuzaliwa kwa CCM. Mji ungepambwa kwa bendera za taifa ingeleta mshikamano na umoja wa Taifa. Kwa bahati mbaya wameahindwa kuona hili.“amesema Msigwa na kutoa tahadhari kwa wafuasi wa CHADEMA na UKAWA.

Hata hivyo niwaase wapenzi na wanachama wa CHADEMA na UKAWA! Wasije uwanjani na nembo au bendera za vyama .Tuonyeshe ukomavu na uelewa wa kisiasa. Michelle Obama aliwahi kusema “when they go low we go high”. Niwaombe tuwakarimu wageni wetu watamani kurudi Iringa tena na tena. Ili tukuze uchumi wa Manispaa yetu.”amesema Msigwa.

Leo Mei 01, 2018 ni siku ya wafanyakazi duniani na maadhimisho ya siku hiyo kitaifa yanafanyika mkoani Iringa na mgeni rasmi ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli.

TRA yakomba fedha zote akaunti ya StarTimes ikidaiwa kodi

0
0
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imechukua fedha zote zilizokuwapo katika akaunti ya kampuni ya StarTimes Tanzania kufidia deni la kodi.

Kampuni ya StarTimes iliyoleta mapinduzi ya matangazo ya digitali nchini tangu kuzimwa kwa mitambo ya analogia kwa mara ya kwanza mwishoni mwa mwaka 2012, inajishughulisha na uuzaji wa ving’amuzi na vifurushi vyake, simu za mkononi na runinga.

Mkurugenzi wa Huduma na Elimu ya Mlipakodi wa TRA, Richard Kayombo alisema jana kwamba mamlaka hiyo imezuia akaunti ya StarTimes kwa sababu ya kushindwa kulipa kodi kwa wakati.

Kayombo alisema akaunti hiyo ilizuiwa kwa siku tatu kabla ya kufunguliwa.

“Ukiona mpaka tumefikia hatua hii ujue suala hilo lilikuwa sugu, hivyo tuliamua kuzuia kwa muda wa siku kama mbili au tatu hivi ili kuhakikisha fedha inapatikana,” alisema.

Kayombo alisema, “Hatukuifungia ila tuliizuia kwani operesheni zake za kuweka ziliendelea kama kawaida, kwa maana ya kuweka fedha isipokuwa walikuwa hawawezi kutoa, lakini sasa tumewafungulia.”

Alisema baada ya siku tatu, mamlaka hiyo ilichukua fedha zote zilizokuwapo na kuiachia akaunti hiyo.

“Katika akaunti tulikuta fedha kiasi lakini pia kwa muda tuliyoizuia kuna nyingine ziliingia, hivyo ilibidi tuchukue zote ili kulipa deni hilo,” alisema.

Hata hivyo, alisema fedha hizo bado hazitoshi kumaliza deni, na kueleza kuwa ni lazima kampuni hiyo ilipe ili kujiweka katika mazingira mazuri ya kufanya biashara.

Alipoulizwa kiasi cha deni inachodai na kilichosalia, Kayombo alisema hiyo ni siri kati ya mamlaka na mteja wake na anayepaswa kutaja kiasi ni mteja.

“Sheria inatukataza kutaja kiasi tunachodai lakini ninachoweza kusema tu kwa sasa ni kweli tumechukua fedha zote baada ya kuzuia akaunti kwa kushindwa kulipa kodi kwa wakati,” alisema.

Alipoulizwa iwapo mamlaka imetoa muda kwa kampuni hiyo kulipa deni lililobaki, Kayombo alisema, “Sheria ya kodi inataka mtu kulipa kodi yake kwa wakati na si vinginevyo.”

Alisema, “Kama wana sababu ya msingi ya kutaka kuongezwa muda, milango yetu ipo wazi, wafuate taratibu na kuja kuzungumza na kamishna wa kodi.”

Awali, ilielezwa kwamba kwa muda mrefu, StarTimes imekuwa ikisuasua katika ulipaji kodi jambo lililosababisha kuonywa mara kadhaa na TRA.

Zitto Kabwe: Tutaendelea kupaza sauti kupigania haki za wafanyakazi

0
0
Mbunge wa Kigoma Mjini na Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe kuwa ataendelea kupaza sauti kupigania haki za wafanyakazi.

Zitto ametumia mitandao yake ya kijamii kueleza hayo, ikiwa leo ni siku ya wafanyakazi amewatakiwa Kila la kheri Wafanyakazi wote nchini huku akiwataka kutimiza wajibu wa kuleta mabadiliko.

"Mei Mosi 2018: Kila la kheri Wafanyakazi wote nchini. Tutimize wajibu wa kuleta mabadiliko

"Licha ya kwamba Wafanyakazi rasmi ni 9% tu ya nguvu kazi ya nchi yetu, ( kwa kigezo cha Kodi ya Mapato ), Wafanyakazi kupitia PAYE wanachangia 75% ya Kodi ya Mapato inayokusanywa na Serikali. Waajiri kupitia kodi za makampuni ( taxes on incomes/interests, profits and capital gains ) huchangia 25% tu.

"Wafanyakazi wanaumizwa na mzigo wa kodi kwa sababu hawana fursa za kukwepa kodi kisheria maana kodi zao hukatwa moja kwa moja kutoka kwenye mishahara yao tofauti na wenye mitaji ambao huweza kukwepa kodi kwa mujibu wa sheria.

"Tutaendelea kupaza sauti kupigania haki za Wafanyakazi, kuhakikisha Uchumi unazalisha ajira rasmi nyingi zaidi na mazingira ya Kazi kuboreka.

"Tunatuma salaam za mshikamano kwa tabaka la Wafanyakazi nchini Katika siku hii muhimu kwao. Wafanyakazi kwenye sekta rasmi wanaofikia 2.1 milioni ni jeshi kubwa la kuleta mabadiliko nchini kwetu. Tutimize wajibu huo.

"Mapambano yanaendelea. Mshikamano daima.

    Kiongozi wa Chama
    ACT Wazalendo
    1/5/2018

Mzee Majuto kupelekwa India leo

0
0
Msanii wa filamu bongo Mzee Majuto leo Mei 1, 2018 anatarajiwa kusafiri na kwenda nchini India kwa ajili ya matibabu zaidi kufuatia matatizo aliyopata siku kadhaa zilizopita.

Steve Nyerere ambaye amehusika kwa namna moja au nyingine katika kusaidia kuratibu zoezi la kumuwezesha Mzee Majuto kwenda nchini India kwa matibabu zaidi amefunguka na kusema kuwa leo Mzee huyo atakwenda kwa matibabu zaidi nchini India na kuwataja watu ambao wamehusika katika kufanikisha jambo hilo na kusema ni pamoja na Rais Dkt. John Pombe Magufuli na Waziri wa Habari Dkt. Harrison Mwakyembe.

"Niseme ahsante sana Mhe. Rais John Pombe Magufuli, Mhe. Mwakyembe, Ummy Mwalimu na wadau pamoja na wasanii mbalimbali kwa kujitoa kwenu, Mzee wetu King Majuto Mungu akipenda leo atakuwa njiani kwenda India kwa matibabu zaidi"

Steve Nyerere hakuishia hapo alikwenda mbali zaidi na kuwataka wasanii wajifunze kupitia kwa Mzee Majuto kuwa kuna ulazima mkubwa wao kuwa na bima ya afya na kusema ni mkombozi kwao, anadai haiwezekani miaka nenda rudi wakawa ni watu wa kuombaomba kila wakati pindi wanapopata matatizo ili hali wanapata pesa za kutosha.

"Tuna kuombea kwa namna moja ama nyingine ,Baba naamini kwa maombi ya Watanzania utarudi katika kazi za ujenzi wa Taifa lako,Kuinua sanaa yetu,Kupeperusha bendera ya mkoa wako ,Baba kuumwa kwako kuna mafunzo mengi kwa wasanii na Watanzania kwa ujumla wake, Wasanii wenzangu bima ya afya ni kitu muhimu kwako na kwa familia yako, Bima ya Afya ni mwokozi kwetu. 

"Sidhani kama miaka nenda rudi tutakuwa watu wa kuomba msaada ,tujiulize tunafanya mapart, tunakunywa na kusaza ,tunajinadi kwenye mitandao nguo zetu kuanzia milioni 3 mpaka 4 tukiulizwa umejipangaje kwa kesho amna kitu, ni muda wa kuamka sasa ,naamini majukumu hayakimbiliki bali tunayakabili" alisisitiza Steve Nyererere

Ajiua kwa kunywa sumu kisa kuachwa na Mke

0
0
MWANAMUME mmoja mkazi wa Katoro mkoani Geita aliyetambulika kwa jina la Maganiko Nunda amejiua kwa kunywa sumu kufuatia mgogoro ulioibuka baina yake na mke wake siku hivi karibuni huku chanzo cha mgogoro huo kikidaiwa kuwa ni unywaji wa pombe kupindukia uliosababisha mkewe kumkimbia.

Akisimulia tukio hilo, mtoto wa marehemu amesema baada ya kwenda kumsalimia baba yake (marehemu) alimkuta ameshafariki huku akitokwa na povu mdomoni na puani.

Marehemu aliacha ujumbe wa barua wenye maneno yasemayo kuwa “…Kwa kuwa nimekuwa kero kwa familia yangu nimeamua kujiua…”

Aidha, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Mponjoli Mwabulambo amethibitisha kutokea kwa kifo hicho japo hakueleza ni aina gani ya sumu ambayo marehemu alitumia kujiua. Jeshi hilo linaendelea na upelelezi wa tukio hilo kabla ya kutoa taarifa kamili kwa umma.

Mwanamke aangua kilio mbele ya Rais Magufuli Iringa....Rais Magufuli atoa maagizo

0
0
Rais John Pombe Magufuli ametoa agizo kwa Mkuu wa Mkoa Iringa pamoja na RPC mkoani humo kumpatia msaada mwanamama Salmakoni Sanga ikiwa ni pamoja na kumpima kama kweli ametolewa kizazi baada ya kudai kushambuliwa na kijana aliyemtaja kwa jina la Mussa.

Rais Magufuli ametoa agizo hilo baada ya kumaliza kuhutubia katika sherehe za Mei Mosi mkoani Iringa ambapo mama huyo alijitokeza na kumlilia Rais Magufuli ampatie msaada kutokana na kunyimwa haki yake mahakamani.

Mama huyo amesema kwamba tukio lake la kushambuliwa na Bw. Mussa lilifanyika mwaka jana ambapo shambulio lilimfanya apoteze kiumbe kilichopo tumboni hali iliyompelekea kutolewa kizazi.

Hata hivyo mama huyo amesema kwamba pamoja na maumivu aliyosababishiwa na kijana huyo, bado mahakama ilimuachia huru mtu huyo na yeye akiamini kwamba alidhulumiwa haki yake na mahakama ya mkoa huo.

Akitoa maagizo, Rais Magufuli amemtaka RPC Iringa Juma Bwire na Mkuu wa Mkoa Bi. Amina Masenza kumtafuta kijana huyo na kumfungulia mashtaka upya hata kama alishinda kesi.

Waziri Mahiga Amuomba Radhi Rais Magufuli

0
0
Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Balozi Augustino Maiga amefunguka na kumuomba radhi Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa niaba ya watu wa Iringa kwa kukosa kura 25 za udhamini katika kipindi cha kampeni za uchaguzi 2015.

Balozi Maiga amesema hayo leo Mei 1, 2018 kwenye maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani ambayo kitaifa inafanyika katika uwanja wa Samora mkoani Iringa ambapo kauli mbiu ya mwaka huu ni Kuunganishwa kwa mifuko ya hifadhi ya jamii kulenge kuboresha mafao ya wafanyakazi"

"Nakumbuka Mhe. Rais ulipata shida kidogo kupata wadhamini hapa Iringa Mjini ikabidi utoke nje ya mji ndiyo ukapata, ila wadhamini 25 kwa hapa mjini kura hazikupatikana tunakuomba radhi sana Mhe. Rais kwa kukosa busara hiyo lakini ulipokuwa hapa ulitoa ahadi kwa wana Iringa na umezitimiza, ahadi ya kwanza ulisema Iringa itakuwa Makao Makuu ya Utalii ya mikoa ya kusini hilo tumeshalifanya, Mkuu wa mkoa aliitisha vikao na watu wa mikoa mingine lakini hasa wewe umeshafanya maamuzi kuwa Uwanja wa ndege wa Iringa wa Nduli utarekebishwa na kuweza kuchukua ndege kubwa zaidi kama zile za Bombidier"

Aidha Maiga aliendelea kusema kuwa

"Na umeshachukua maamuzi kwamba barabara ya kutoka hapa Iringa kwenda hifadhi ya Ruaha itakuwa katika kiwango cha lami mara nyingi na mimi nimekuwa nakuomba na kukukumbusha kuhusu maendeleo ya mkoa wa Iringa, umenisikiliza na kutekeleza hapa Iringa pekee yake mjini barabara zimetengenezwa kwa kutumia bilioni 6.4, shule kongwe kwama vile Tosamaganga, Malangali zimeboreshwa, miradi ya afya na maji ni mabilioni siwezi kusema lakini kubwa kabla ya kufika hapa umefungua barabara kuu ya Afrika ya Kati na Afrika Mashariki, barabara hii inapita katikati ya mkoa wa Iringa juzi pale Isimani umesema barabara hii iwe mkombozi kwa watu wa Iringa"

Tucta wamuomba Rais kuongeza mshahara kima cha chini

0
0
Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) limemuomba Rais John Magufuli kuangalia namna ya kuongeza mshahara wa kima cha chini angalau kisiwe chini ya Sh250, 000.

Hayo yamesemwa leo Mei Mosi na Katibu Mkuu wa Tucta, Dk Yahaya Msigwa wakati wa sherehe za wafanyakazi, zinazoadhimishwa kitaifa katika viwanja vya Samora mkoani Iringa, ambapo Mgeni Rasmi ni Rais John Magufuli.

Amesema maisha kwa walio wengi yanakuwa magumu kutokana na kupanda kwa bei za vitu muhimu ikiwemo vyakula na huduma za msingi za maisha.

“Tunaomba Rais wetu kima cha chini kisipungue 250,000 kwa mwezi , lakini pia tunaiomba Serikali kubuni vyanzo vingine vya mapato ili kuongeza wigo wa utoaji huduma kwa watumishi au wafanyakazi, kuna mfanyakazi anapata Sh100,000 hii haitoshi kitu kwa mtu mwenye familia yenye watoto wanne,” amesema Dk Msigwa.

Aidha alitoa wito kwa Serikali kuangalia upya namna ya kubuni vyanzo vingine vya mapato ili kupunguza machungu kwa wafanyakazi kwani wanakatwa kodi kubwa.

Rais Magufuli Awaonya Wakurugenzi

0
0
Rais John Magufuli ameagiza kuchukuliwa hatua kwa wakurugenzi wanaowanyima haki zao wafanyakazi kwa kuwahamisha bila kuwalipa posho ya uhamisho.

Ameyasema hayo mkoani Iringa leo katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi duniani, ambayo kitaifa yamefanuika mkoani humo.

“Ukimuhamisha mtumishi mlipe fedha yake kabla ya kumuondoa na hili nalisema kwa mara ya mwisho sitarudia tena kulizungumza hilo katika maisha yangu.

“Leo nimeona bango jingine nafikiri chama cha walimu kinachosema wao wanaendelea kuhamishwa bila kulipwa fedha za uhamisho, najua viongozi wanaosimamia wizara zinazohamisha wako hapa, kama kuna mtu yeyote anahamisha bila kulipa huyo ni jeuri na dawa yake ni kumtoa”, amesema Rais Magufuli.

Pamoja na mambo mengine, Rais Magufuli amewataka wananchi wa Iringa na Njombe kuchukua tahadhari juu ya ugonjwa wa Ukimwi kutokana na mikoa hiyo miwili kuongoza kwa ugonjwa huo nchini.

Ahadi ya Rais Magufuli Kwa Wafanyakazi Baada ya Kushindwa Kuwapandishia Mishahara Mwaka Huu

0
0
Katika hotuba yake leo kwenye maadhimisho ya Siku ya wafanyakazi (Mei Mosi), yaliyofanyika kitaifa Mkoani Iringa, Rais Magufuli ameahidi kupandisha mishahara kwa kiasi kikubwa kabla hajamaliza awamu yake ya uongozi.

''Kipindi changu cha Urais hakitaisha kabla sijapandisha mishahara wafanyakazi. Na mimi nataka niwaeleze kupandisha kwangu kutakuwa si kwa elfu kumi, kutakuwa kupandisha kwelikweli'', amesema Rais Magufuli.

Aidha Rais Magufuli ameweka wazi kuwa alitamani sana mwaka huu kupandisha mishahara lakini baada ya kuona changamoto zilizopo ikiwemo kulipa madeni ya nyuma akaona azimalize kwanza kabla ya kupandisha.

"Natamani mwaka huu kupandisha mishahara kwa wafanyakazi lakini kutokana na changamoto zilizopo za kuajiri wafanyakazi 52,000 nitawalipa nini? nikisema natamka kuongeza mishahara, nitazipata wapi?”amesema Magufuli.

Pamoja na hayo Rais Magufuli ameviomba vyama vya wafanyakazi na masharikisho yao, kuendelea kuiunga mkono serikali ya awamu ya tano kwasababu inaongozwa na walimu akiwemo yeye mwenyewe na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ambao wote wamewahi kuwa walimu.

Pia Rais Magufuli amemshukuru Rais wa Shirikisho la Vyama Vya Wafanyakazi (TUCTA)  Tumaini Nyamhokya, kwa maandalizi mazuri ya sherehe hizo ambazo zimefanyika kwenye uwanja wa Samora mjini Iringa.

Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini (TMA) yatoa tahadhari ya mvua Kubwa Mikoa Mitano

0
0
Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini (TMA) imetoa tahadhari ya kunyesha mvua kubwa juu ya wastani, kwa siku tano zinazoweza kusababisha mafuriko katika maeneo mengi nchini .

Kwa mujibu wa TMA, mvua hizo zitaanza leo Mei Mosi mpaka Mei 5 mwaka huu na zinatarajiwa kunyesha mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Tanga pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba.

Mikoa mingine ni Mara, Mara, Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Tabora, Katavi, Kigoma, Arusha, Kilimanjaro na Manyara.

TMA imesema kiwango cha athari zinazoweza kutokea katika jamii ni pamoja na adha ya usafiri, barabara kubwa kutopitika na maji kujaa au kupita kwa kasi.

Pia imetoa wito kwa wakazi wa maeneo ya mabondeni kuchukua tahadhari stahiki na kuendelea kufuatilia taarifa pamoja na tahadhari zitakazotolewa.

Habari Zilizopo Katika Magazeti Ya Leo Jumatano ya May 2

Viewing all 45270 articles
Browse latest View live




Latest Images